-Asisitiza utekelezaji wa maono ya Rais ya kujenga uchumi shindani, bidhaa bora kuvutia masoko ya ndani na kimataifa.

-Atoa rai kwa TBS kuimarisha viwango na kutoa elimu kwa wazalishaji ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania.

-Asema Serikali inaendelea kuimarisha maabara, mifumo ya ukaguzi, upimaji na uthibitishaji wa bidhaa.

-Awaasa washindi wa tuzo za ubora kulinda chapa zao na kuzalisha bidhaa zenye viwango bora.

DAR ES SALAAM

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (Mb), ametoa Tuzo za Ubora za Kitaifa za mwaka 2026 zilizoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwenye hafla ya Usiku wa Viwango na Tuzo za Ubora iliyofanyika Serena Hotel jijini Dar es Salaam.

Waziri Kapinga ametoa tuzo kwa wadau mbalimbali waliofanya vizuri katika kuzingatia na kuendeleza viwango vya ubora, huku akielekeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuendelea kuboresha viwango vya bidhaa ili kuongeza ushindani wake katika masoko ya ndani na kimataifa, kwani hatua hiyo ni sehemu ya kutekeleza maono ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kujenga uchumi shindani kupitia uzalishaji wenye tija na ubora.

Amesisitiza kuwa uzalishaji wa bidhaa nyingi unapaswa kwenda sambamba na ubora unaokidhi mahitaji ya soko na uwezo wa kushindana na bidhaa nyingine na kuahidi kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya ubora ikiwemo maabara, mifumo ya ukaguzi, upimaji na uthibitishaji wa bidhaa, ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na zinazoingizwa nchini zinakidhi matakwa ya ubora na usalama.

Aidha, ametoa rai kwa TBS kuwa makini na mabadiliko ya viwango katika masoko ya nje na kuchukua hatua za mapema kuwaandaa wazalishaji wa ndani kukidhi matakwa hayo kwa lengo la kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kuielekeza TBS kuendelea kutoa elimu na ujuzi wa kitaalamu kwa wazalishaji, kuhamasisha matumizi ya teknolojia fanisi na nishati safi pamoja na kushirikiana na taasisi nyingine katika kuimarisha ubora wa bidhaa.

Pia amewaasa wafanyabiashara kuona viwango kama uwekezaji badala ya gharama, huku akihimiza matumizi ya bidhaa za kitanzania kwa kutumia chapa ya utambulisho ya "Made in Tanzania".

Waziri Kapinga amewapongeza washindi na kuwataka kuendelea kuboresha bidhaa na huduma zao ili kulinda chapa zao na kudumisha viwango vya ubora na kusema kuwa Tanzania imeonesha uwezo wa kufanya vizuri katika tuzo za ubora za kikanda, hususan katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), hivyo juhudi hizo zinapaswa kuendelezwa ili kuitangaza nchi na bidhaa zake katika masoko ya kimataifa.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Sempeho Manongi, amesema uwekezaji katika viwango ni uwekezaji katika ushindani na upanuzi wa masoko, akisisitiza kuwa bei nzuri inaweza kumvutia mteja mara moja, lakini ubora ndiyo unaomfanya arudi tena na tena na kuongeza kuwa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania inalenga kujenga utambulisho wa bidhaa zinazotambulika kwa ubora na kuwa fahari ya taifa katika masoko ya dunia.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt Ashura Katunzi, amesema,viwango ni muhimu katika kulinda afya na usalama wa wananchi, kuimarisha biashara na kuwezesha bidhaa za Tanzania kufikia masoko mbalimbali.ma amesisitiza kuwa viwango si nyaraka bali ni uchumi, maisha na biashara, huku akisisitiza kuwa TBS hutumia kamati za kitaalamu kuandaa na kuboresha viwango na kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia mafunzo, mijadala na maonesho kuhusu ubora na nishati safi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TBS, Prof. Othman Chande, amesema kujenga taifa lenye ushindani kunahitaji uongozi wenye maono, mifumo imara ya usimamizi, uwajibikaji na utamaduni wa kuzingatia ubora. na kuongeza kuwa bodi itaendelea kusimamia utawala bora, uwazi na ubunifu wa menejimenti pamoja na kuunga mkono juhudi za watendaji katika kuongeza ufanisi wa shirika.

Hafla hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Viwango Duniani na imeambatana na utoaji wa Tuzo za Ubora za Kitaifa za mwaka 2026 kwa lengo la kutambua mchango wa wadau mbalimbali na viongozi wa kamati za kitaalamu waliotumikia kwa zaidi ya miaka 15 na yamelenga kuhamasisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kujenga utamaduni wa ubora utakaoongeza thamani ya bidhaa, kupanua masoko, kukuza biashara na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: