TÜRKİYE, Novemba 26, 2026
Tanzania inashiriki katika Mkutano wa 13 wa Tume za Taifa za UNESCO kutoka Kanda mbalimbali duniani, unaofanyika leo Novemba 26–27, 2026 jijini Ankara, Türkiye. Ushiriki wa Tanzania umewakilishwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Hamisi Masanja Malebo. Lengo la mkutano huu ni kujadili nafasi na mchango wa Tume za UNESCO katika kuendeleza dhamira na vipaumbele vya UNESCO katika nchi wanachama.
Mkutano huu umewakutanisha wawakilishi wa Tume za Taifa za UNESCO kutoka maeneo mbalimbali duniani ili kujadili majukumu yao, kubadilishana uzoefu na kutafuta njia za kuimarisha uratibu wa shughuli za UNESCO katika ngazi za kitaifa na kimataifa.
Tume za Taifa za UNESCO zina jukumu muhimu la kuunganisha shughuli za UNESCO na vipaumbele vya maendeleo ya nchi wanachama. Kupitia uratibu na ushirikishwaji wa taasisi za serikali pamoja na wadau mbalimbali, Tume hizi huchangia katika utekelezaji wa programu za UNESCO katika maeneo ya elimu, sayansi, utamaduni, mawasiliano na habari.
Kwa Tanzania, ushiriki katika mkutano huo ni fursa ya kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi nyingine, kuimarisha mahusiano ya kitaasisi na kupata maarifa yanayoweza kutumika kuboresha uratibu na utekelezaji wa programu za UNESCO nchini.
Mkutano huu unafanyika kwa mfumo mseto, unaowawezesha washiriki kuhudhuria ana kwa ana jijini Ankara au kushiriki kwa njia ya mtandao, hivyo kupanua wigo wa ushiriki wa Tume za Taifa kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Ushiriki huu unaendana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha diplomasia, kupanua wigo wa ushirikiano wa kimataifa na kukuza mahusiano na jumuiya ya kimataifa. Mwelekeo huo unasisitizwa pia katika Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania, inayoweka mkazo katika ushiriki madhubuti wa nchi katika taasisi za kikanda na kimataifa kwa ajili ya kulinda na kuendeleza maslahi ya taifa.
Kupitia ushiriki Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuimarisha uhusiano kati ya UNESCO na wadau wa kitaifa, sambamba na kukuza utekelezaji wa programu zinazochangia maendeleo ya nchi katika maeneo mbalimbali ya kazi za Shirika hili.
#UNESCOTanzania #UNESCO #Tanzania #NationalCommissionsForUNESCO #Ankara2026 #InternationalCooperation #Elimu #Sayansi #Utamaduni #MawasilianoNaHabari



Post A Comment: