Na John Mapepele, Dodoma

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewataka Watanzania kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Waziri Mchengerwa ametoa wito huo leo katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), yaliyoambatana na mbio za NHIF Marathon 2026 zilizoshirikisha takribani watu 10,000.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mchengerwa amesema Serikali imetoa takribani Shilingi bilioni 98 kuwawezesha wananchi wasio na uwezo kupata huduma za afya kupitia mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.

Amesema Serikali pia imekuja na kifurushi cha bima ya afya cha Shilingi 150,000 kwa kaya, kinacholenga makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo wakulima, wafanyakazi, waendesha bodaboda, wafugaji na wafanyabiashara wadogo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kifurushi hicho kinamwezesha mwanachama kuchangia wastani wa Shilingi 25,000 kwa mwaka na kupata huduma kwa kipindi cha miezi 12.

Ameeleza kuwa kifurushi hicho kinatoa huduma takribani 372 katika ngazi mbalimbali za vituo vya afya, zikiwemo zahanati, vituo vya afya, hospitali za halmashauri, hospitali za mikoa, hospitali za rufaa, hospitali za kanda na hospitali ya taifa.

Aidha, amesema magonjwa yasiyoambukiza yanachukua zaidi ya asilimia 37 ya matumizi ya jumla ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kufanya mazoezi na kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini viashiria vya magonjwa kama kisukari, magonjwa ya moyo na saratani.

"Ndugu zangu Watanzania, tunapoelekea kwenye Dira ya Taifa 2050, tunakusudia kila Mtanzania kuwa na afya njema. Lakini afya njema inategemea na mambo kadhaa. Kwanza, hamasa ya mazoezi ni lazima iwe kubwa. Na ni mategemeo yangu kwamba wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya watahamasisha Watanzania kufanya mazoezi. Mazoezi ya kila siku, mazoezi ya wiki, mazoezi ya mwezi. Mazoezi haya yatatusaidia kwenda kupunguza magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza. Mzigo mkubwa unaoikuta Bima ya Afya kwa Wote kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza ambayo leo hii yanachukua zaidi ya asilimia 37 ya matumizi ya jumla ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, zaidi ya asilimia 37." amefafanua Mhe. Mchengerwa.

Ameongeza kuwa Rais Samia anataka kila Mtanzania kuwa na kadi ya bima ambapo kwa sasa amekuja na kifurushi cha shilingi 150,000. Kifurushi kinachomsaidia kila mtanzania: bodaboda, mama ntilie, wafugaji, na mkulima.


Mhe. Mchengerwa amesema Baba wa Taifa alipozungumzia kuhusu maadui watatu, ujinga, maradhi na umaskini, alikusudia kila mtanzania kuwa na afya njema.

" Lakini eneo hili sasa Daktari Samia ameongeza kasi ya utekelezaji wa maazimio aliyoyatoa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Katika elimu tunashuhudia. Na katika afya msingi wake aliujenga na kuuweka kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2025/2030 katika ibara ya 38 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi". Amefafanua Mhe Mchengerwa

Katika hatua nyingine, Mchengerwa amewaelekeza madaktari, wauguzi na wataalamu wa afya katika vituo zaidi ya 13,000 nchini kuwaelimisha wagonjwa kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya.

Amesema wahudumu wa afya wanapaswa kuwauliza wagonjwa kama wana vitambulisho vya bima na kuwashauri wale ambao hawana kuhusu faida za kujiunga na huduma hiyo.

Pia ameitaka menejimenti ya NHIF kuboresha mifumo ya kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho vya bima na kuhakikisha fidia kwa wadau wa huduma za afya inalipwa kwa wakati.

Maadhimisho hayo yamehitimishwa kwa mbio za kilomita 21, kilomita 10 na kilomita 5, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea miaka 25 ya NHIF na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa mazoezi ambapo Mhe. Mchengerwa alikimbia mbio za kilomita 10.

Katika maadhimisho hayo, washindi walipewa tuzo, vyeti na fedha taslimu ambapo pia wasanii wa kizazi kipya wakiongoza na Hamonize walitoa burudani.



Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: