Na Manish Govindji, Afisa Mtendaji Mkuu wa Liquid Intelligent Technologies Tanzania
Uzinduzi wa waraka wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 tarehe 3 Agosti umeweka msisitizo mpya kuhusu nafasi ya sekta ya biashara katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya nchi.
Mwezi Agosti, Rais Samia Suluhu Hassan alipozindua nyenzo za utekelezaji, ufuatiliaji na kuharakisha maendeleo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, ushirikiano imara zaidi kati ya Serikali na sekta binafsi ulikuwa miongoni mwa masuala yaliyopewa kipaumbele. Sekta ya biashara inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika uwekezaji, uzalishaji wa ajira, ubunifu na ukuaji wa uchumi.
Uzinduzi huo ulifuatia kutangazwa rasmi kwa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 jijini Dodoma mwezi Julai 2025, na ulihusisha pia kusainiwa kwa Tamko la Pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi. Ahadi hiyo inalenga kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano wakati Tanzania ikielekea kufikia uchumi wa dola trilioni moja za Marekani na kipato cha wastani cha dola 7,000 za Marekani kwa kila mwananchi ifikapo mwaka 2050.
Nafasi ya sekta binafsi
Inatarajiwa kuwa takribani asilimia 70 ya utekelezaji wa Dira 2050 utatokana na sekta binafsi, jambo linaloweka wajibu kwa kampuni zinazofanya biashara nchini Tanzania kutathmini namna uwekezaji na uwezo wao unavyoweza kuchangia katika kufikia malengo ya uchumi wa taifa.
Hali hii inatoa fursa, lakini pia inaleta wajibu. Kwa kampuni za teknolojia kama Liquid Intelligent Technologies Tanzania, wajibu huo unajumuisha kusaidia kujenga miundombinu, ujuzi na uwezo wa kidijitali ambao biashara zinahitaji ili kukua na kushindana katika uchumi wa kidijitali.
Uzalishaji, uwekezaji, ajira na ubunifu ni mambo muhimu katika azma ya Dira 2050 ya kuifanya Tanzania kuwa uchumi shindani wenye kipato cha juu. Teknolojia ya kidijitali inaweza kusaidia kufanikisha malengo hayo kwa kuwezesha biashara kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, kupanua shughuli zake na kushindana katika masoko ya ndani na ya kikanda.
Ingawa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupanua upatikanaji wa huduma za kidijitali, changamoto inayofuata ni kubadilisha upatikanaji huo kuwa shughuli za kiuchumi zenye matokeo yanayopimika.
Miundombinu ya mawasiliano na muunganisho wa kidijitali bado ni msingi muhimu, lakini mageuzi ya kidijitali sasa yamevuka hatua ya kuunganisha biashara pekee. Kampuni zinazidi kutegemea mifumo ya huduma za wingu (cloud), usalama wa mtandao, huduma za data na nyingine za kidijitali ili kuongeza uzalishaji na kufikia masoko mapya. Miundombinu ya kidijitali inazidi kuwa sehemu muhimu ya miundombinu ya uchumi.
Teknolojia kama kichocheo cha ukuaji
Miongoni mwa vikwazo vilivyobaki ni namna baadhi ya taasisi zinavyoitazama teknolojia. Biashara nyingi bado zinaona mageuzi ya kidijitali kama gharama badala ya kuwa kichocheo cha ukuaji. Taasisi zinazofanya vizuri zaidi ni zile zinazotumia teknolojia kuboresha huduma bora wa wateja, ufanisi, ufanyaji wa maamuzi na uwezo wa kushindana.
Kama sehemu ya makampuni ya Cassava Technologies, Liquid inahudumia zaidi ya biashara 2,000 nchini Tanzania kupitia mfumo jumuishi wa huduma za kidijitali unaojumuisha muunganisho wa mawasiliano, vituo vya kuhifadhi na kuchakata data, huduma za wingu, usalama wa mtandao, suluhisho za akili unde (AI) na huduma za malipo. Uzoefu wahuduma hizi unaipa kampuni uelewa wa vikwazo halisi vinavyokabili taasisi, ikiwemo upungufu wa ujuzi, wasiwasi kuhusu usalama wa data na mifumo, pamoja na kutokuwa na uhakika kuhusu namna uwekezaji katika teknolojia ya kidijitali utakavyoboresha shughuli zao.
Upitishaji wa teknolojia pia unategemea mazingira mapana yanayoiwezesha. Upatikanaji wa umeme wa uhakika, muunganisho wa mawasiliano, mifumo salama na huduma za malipo ya kidijitali zinazopatikana kwa urahisi ni muhimu ili biashara ziweze kuwekeza kwa kujiamini na kutumia zana za kidijitali kwa ufanisi.
Uwezo wa rasilimali watu ni muhimu vilevile
Sekta binafsi pia ina wajibu wa kusaidia kukuza watu watakaounda na kuendesha uchumi wa kidijitali. Tanzania itahitaji ujuzi mbalimbali wa kidijitali, pamoja na ubunifu, ujasiriamali na uwezo wa kutatua changamoto.
Liquid Tanzania inachangia katika eneo hili kupitia programu kama ProjeKt Inspire, inayotoa mafunzo ya vitendo katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) kupitia shughuli zinazofanyika shuleni, programu za vijana, maendeleo ya walimu na nyenzo za kujifunzia. Kampuni pia imeunga mkono Tuzo za TEHAMA, zinazotambua mafanikio na ubunifu katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano nchini Tanzania, na kutoa fursa kwa vipaji vya ndani na suluhisho za kiteknolojia kutambulika zaidi.
Mipango hii inaonesha namna ushiriki wa sekta binafsi unavyoweza kwenda zaidi ya uwekezaji wa mitaji na kujumuisha kukuza ujuzi na uwezo wa ubunifu unaohitajika kwa maendeleo ya uchumi ya muda mrefu.
Kufikia uwezo halisi wa Tanzania
Kwa kuangalia mbele, Tanzania ina uwezo wa kuwa kitovu kinachoongoza cha huduma za kidijitali katika Afrika Mashariki na Kati, ikiwa na fursa ya kutoka katika nafasi ya kuwa mtumiaji mkuu wa teknolojia na kuwa mzalishaji na msafirishaji wa huduma za kidijitali.
Kosa kubwa litakuwa kuzingatia huduma za kidijitali bila kuimarisha misingi inayozitegemeza. Mageuzi ya kidijitali lazima yawe jumuishi, ya gharama nafuu na yaungwe mkono na ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na watoa huduma za teknolojia.
Kwa sekta binafsi, hapo ndipo mabadiliko kutoka kwenye matarajio na mipango kwenda kwenye utekelezaji yanapoweza kuonekana kwa vitendo. Kufikia matarajio ya Dira 2050 kutahitaji kampuni si tu kutumia fursa mpya zinazojitokeza, bali pia kuwekeza katika miundombinu, ujuzi na uwezo wa kibiashara unaowezesha fursa hizo kufikiwa na kuleta matokeo halisi.



Post A Comment: