NA EMMANUEL MBATILO DAR ES SALAAM

Serikali imeipongeza GS1 Tanzania kwa kuwezesha wazalishaji zaidi ya 7,000 kuingiza bidhaa zao katika maduka makubwa na masoko ya kimataifa kupitia mifumo ya utambuzi wa bidhaa, ikiwemo barcode na QR Code, hatua inayochochea ukuaji wa biashara na ushindani wa bidhaa za ndani.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Rajab Salum, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi amesema mifumo ya utambuzi na ufuatiliaji wa bidhaa ina mchango mkubwa katika kuboresha ufanisi wa minyororo ya ugavi, kuongeza uwazi wa taarifa za bidhaa na kurahisisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amesema mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya viwanda na biashara, hususan kuwawezesha wazalishaji wadogo, wadogo sana na wa kati kushiriki katika mifumo rasmi ya masoko.

Ameongeza kuwa GS1 Tanzania imekuwa na mchango katika kuendeleza mifumo ya utambuzi wa bidhaa nchini tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011, hususan kupitia matumizi ya barcode na teknolojia nyingine zinazowezesha taarifa za bidhaa kupatikana kwa urahisi.

Amesema mifumo hiyo inasaidia kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa, huku ikirahisisha ufuatiliaji wa bidhaa katika hatua mbalimbali za mnyororo wa ugavi.

Katika hatua nyingine, Serikali imeihimiza GS1 Tanzania kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo kuhamia kutoka barcode za 1D kwenda teknolojia za 2D, ili kuongeza upatikanaji wa taarifa za bidhaa na kuimarisha uwazi katika biashara.

Amesema mabadiliko hayo yanapaswa kwenda sambamba na elimu kwa wazalishaji, wafanyabiashara na watumiaji, pamoja na kuwajengea uwezo wadau wote ili waweze kutumia teknolojia hizo kwa ufanisi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa GS1 Tanzania kupanua huduma zake katika sekta nyingine zikiwemo afya, ujenzi, kilimo na usafirishaji, akieleza kuwa matumizi ya mifumo ya utambuzi na ufuatiliaji wa bidhaa yana nafasi kubwa katika kuongeza ufanisi wa sekta hizo.

Amesema Serikali inatambua kuwa maendeleo ya viwanda na biashara yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za umma, sekta binafsi, taasisi za viwango na mamlaka za udhibiti ili kujenga mazingira bora ya uzalishaji na biashara.

Katika hilo, ameieleza GS1 Tanzania umuhimu wa kuendelea kushirikiana na TBS, TIRDO na taasisi nyingine za Serikali katika kuimarisha matumizi ya viwango, ufuatiliaji wa bidhaa na ujenzi wa uwezo wa wazalishaji.

Pia amewataka wanachama kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Bodi mpya kwa kuzingatia Katiba na taratibu za taasisi, akieleza kuwa uongozi huo unapaswa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kusimamia utekelezaji wa mpango kazi huo.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: