SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imesema itaendelea kwenda hatua ya ziada katika kuboresha huduma kwa wateja kwa kutumia teknolojia, kuongeza kasi ya utatuzi wa changamoto na kuimarisha mifumo ya kupokea na kufanyia kazi mrejesho wa wateja.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TTCL, Bi. Anita Moshi, wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Huduma kwa Mteja 2026 uliofanyika katika Kituo cha Kijitonyama FTTX Experience Center.
Moshi amesema katika dunia ya sasa yenye maendeleo ya haraka ya teknolojia, ushindani wa biashara haupimwi kwa bei au aina ya bidhaa pekee, bali pia ubora wa uzoefu anaoupata mteja.
Amesema huduma kwa mteja si jukumu la kitengo kimoja pekee, bali ni wajibu wa kila mfanyakazi wa TTCL, kuanzia wahandisi wanaohakikisha mtandao unafanya kazi vizuri hadi maafisa wanaopokea simu na viongozi wanaofanya maamuzi.
Amesema kaulimbiu ya Wiki ya Huduma kwa Mteja mwaka huu, “The Extra Mile” (Hatua ya Ziada), inalenga kuhamasisha wafanyakazi kuwa tayari kwenda zaidi ya matarajio ya mteja kwa kutambua na kutatua changamoto kabla hazijaleta malalamiko.
“Kwetu TTCL, kwenda hatua ya ziada maana yake ni kuwa proactive kwa kutambua na kutatua changamoto kabla mteja hajalalamika, kutotoa majibu tu bali kutoa suluhisho la kudumu na kutokuchukulia malalamiko kama kero, bali kama fursa ya kujifunza na kuboresha mifumo yetu,” amesema.
Amesema TTCL itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwamo huduma ya Faiba Mlangoni Kwako, huku ikisisitiza kuwa teknolojia bora lazima iendane na huduma bora kwa wateja.
Aidha, amesema kila mfanyakazi anatakiwa kuwa balozi chanya wa taswira ya TTCL, huku kampuni ikiweka mazingira wezeshi na kutoa zana sahihi za kazi kwa wafanyakazi ili waweze kutoa huduma bora.
Moshi amewashukuru wateja kwa kuendelea kuamini huduma za TTCL, akiahidi kuwa kampuni hiyo itaendelea kuwasikiliza na kuboresha huduma zake ili kukidhi matarajio yao.
Amewataka wafanyakazi kuzingatia kaulimbiu hiyo katika utendaji wao wa kila siku akisema: “Kila mteja. Kila huduma. Kila siku. Twende hatua ya ziada.”
Ametangaza rasmi kuanza kwa Wiki ya Huduma kwa Mteja 2026 yenye kaulimbiu “The Extra Mile – Huduma Bora, Hatua ya Ziada kwa Mteja.”










Post A Comment: