Afisa Matekelezo Mfuko wa PSSSF Josephine Nyamtondo, akimsaidia mstaafu Bi. Sara Banali, kujihakiki kwenye ofisi ya PSSSF Kibaha Mkoani Pwani, Oktoba 7, 2026 wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yakiingia siku ya tatu

Watumishi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Kituo cha Afya Mkoani Mjini Kibaha baada ya kuwakabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja Mjini Kibaha Pwani Oktoba 7, 2026


Afisa Mfawidhi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Mkoa wa Pwani, Bw. John Mwalisu (Mwenye suti nyeusi kulia), akimkabidhi Dkt. Ephraim Tahhan, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mkoani Mjini Kibaha Pwani, msaada wa mahitaji mbalimbali uliotolewa na Watumishi wa PSSSF Mkoani Pwani, kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Oktoba 7, 2026.

Afisa Mfawidhi wa Mfuko wa Psssf Mkoa wa Pwani, Bw. John Mwalisu, akizungumza na wanachama wa PSSSF waliotembelea ofisi za Mfuko Mjini Kibaha, huo Oktoba 7, 2026 wakati wa maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja.


Afisa Mfawidhi wa Mfuko wa PSSSF Mkoa wa Pwani, Bw. John Mwalisu, akizungumza na wanachama wa PSSSF waliotembelea ofisi za Mfuko Mjini Kibaha, huo Oktoba 7, 2026 wakati wa maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja.

Na Mwandishi Wetu, Kibaha

Afisa Mfawidhi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Mkoa wa Pwani, Bw. John Mwalisu, amewakumbusha wanachama wa Mfuko huo kuwa huduma zote za PSSSF zinapatikana kupitia ofisi za Mfuko na njia rasmi za huduma, huku akisisitiza kuwa PSSSF haina mawakala wanaofanya kazi kwa niaba yake.

Bw. Mwalisu ametoa kauli hiyo Oktoba 7, 2026, wakati akiwashukuru wanachama wa PSSSF waliotembelea ofisi za Mfuko mjini Kibaha, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja.

“PSSSF hatuna mawakala. Taarifa sahihi kuhusu huduma za Mfuko utazipata moja kwa moja kutoka PSSSF. Aidha, hakuna huduma yoyote ya PSSSF inayolipiwa; huduma zetu zote ni bure. Hata wazee ambao hawana uwezo wa kufika ofisini kwa ajili ya kuhakiki taarifa zao, tunawafuata hadi majumbani kwao,” alisema Mwalisu.

Katika tukio hilo, wanachama wa PSSSF, wakiwemo maafisa kutoka Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na watoa huduma za afya, walipata fursa ya kufahamu zaidi kuhusu majukumu ya Mfuko, huduma zinazotolewa na maboresho mbalimbali yaliyofanywa ili kuongeza ufanisi na kuendana na mahitaji ya wakati.

Akizungumzia maboresho hayo, Mwalisu alisema PSSSF inaendelea kutekeleza kaulimbiu ya “Tunalipa Jana”, inayolenga kuhakikisha mwanachama anayestaafu anapata stahiki zake kwa wakati na bila kuchelewa.

“Kwa sasa PSSSF tunakwenda na kaulimbiu ya ‘Tunalipa Jana’, ikiwa na maana kwamba mwanachama anapostaafu, stahiki zake anazipata mara moja,” alisema.

PSSSF YAENDA ‘EXTRA MILE’ KUWAFIKIA WANACHAMA

Katika hatua nyingine, watumishi wa PSSSF Mkoa wa Pwani wameenda “Extra Mile” kwa kuwatembelea wanachama wao katika Kituo cha Afya cha Mkoani kilichopo Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Msafara huo uliongozwa na Afisa Mfawidhi wa PSSSF Mkoa wa Pwani, Bw. John Mwalisu, na kupokelewa na Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dkt. Ephraim Taahani.

Katika ziara hiyo, PSSSF ilikabidhi mahitaji mbalimbali kwa ajili ya watumishi wa kituo hicho ambao pia ni wanachama wa Mfuko huo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Bw. Mwalisu aliwashukuru watumishi wa kituo hicho kwa kuendelea kutoa huduma bora za afya kwa wananchi, wakiwemo wanachama wa PSSSF.

Alisema mchango wa watumishi hao ni muhimu katika kujenga jamii yenye afya na kuchochea maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Dkt. Taahani aliishukuru PSSSF kwa kutambua mchango wa wahudumu wa afya katika jamii kupitia ziara hiyo na utoaji wa mahitaji muhimu.

Aliahidi kuhakikisha kuwa mahitaji hayo yanawafikia pia watumishi wengine ambao walikuwa wakiendelea kuwahudumia wagonjwa wakati wa ziara hiyo.

Aidha, uongozi wa kituo hicho ulieleza kuwa una imani na namna PSSSF inavyosimamia fedha na maslahi ya wanachama wake, huku ukipongeza juhudi za Mfuko katika kuboresha huduma na kuwafikia wanachama wake.

MWISHO

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: