Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Taasisi ya Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), hatua inayolenga kuunganisha nguvu katika kutatua changamoto za kijamii kupitia Sayansi, Takwimu na Teknolojia.
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo,Makamu Mkuu wa NM-AIST Profesa Maulilio Kapanyula amesema NM-AIST ni kitovu cha ubunifu na Ugunduzi na imekuwa ikizalisha teknolojia mbalimbali zinazolenga kuleta majibu ndani ya jamii.
Amesema taasisi imefanikiwa kubuni teknolojia za kisasa,ikiwemo teknolojia ya kugundua uvujaji wa maji na teknolojia ya kubaini maeneo ambapo umeme umekatika, ambazo zinahitaji takwimu sahihi na uchambuzi wa kitaalamu kutoka EASTC ili kufanyiwa majaribio na kutathminiwa kabla ya kupelekwa kwa jamii.
"Tumekuwa na bunifu nyingi lakini ili zifike sokoni na kuleta tija tunahitaji ushirikiano,Wenzetu wa EASTC ni wabobezi katika ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu, hivyo makubaliano haya yatatusaidia kufanya validation ya bunifu zetu kwa kutumia data halisi," alisema.
Aliongeza kuwa ushirikiano huo utajikita pia katika maeneo ya sayansi ya data, upangaji wa miji kwa kutumia takwimu,pamoja na usambazaji wa huduma za maji na nishati kwa kutumia mifumo ya kidijitali.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, taasisi hizo mbili zitaendesha tafiti za pamoja,kubadilishana wataalamu na wanafunzi, pamoja na kuhakikisha bunifu zinazozalishwa zinawafikia wananchi na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Profesa Tumaini Katunzi wa Taasisi ya Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) amesema ushirikiano kati ya taasisi yake na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) unalenga kuhakikisha takwimu na teknolojia vinatumika moja kwa moja kutatua kero za wananchi.
Alisema EASTC ni Taasisi inayoongoza kwa ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu ukanda wa Afrika Mashariki, imekuwa na changamoto ya kutumia teknolojia za kisasa katika kuchakata takwimu hizo.
"Sisi tuna takwimu, wenzetu wa Nelson Mandela wana teknolojia na bunifu. Tukichanganya nguvu tutapata majibu ya changamoto za maji kupotea, umeme kukatika na upangaji mbovu wa miji kwa kutumia data halisi," alisema Prof. Katunzi.
Ushirikiano huo utahusisha tafiti za pamoja, kubadilishana watafiti, na kujenga uwezo kwa wanafunzi katika fani ya Sayansi ya Takwimu na Ubunifu huku utiaji saini wa makubaliano hayo unatajwa kuwa hatua muhimu kuelekea uchumi unaoongozwa na sayansi na data nchini.
















Post A Comment: