MLANDIZI, PWANI
BRIGEDIA Jenerali David Msakulo amewataka wazazi kushirikiana kwa karibu na walimu na walezi katika malezi ya watoto ili kuwajenga kuwa viongozi bora wa taifa.
Msakulo alitoa kauli hiyo wakati wa mahafali ya wanafunzi wa darasa la Awali katika Shule ya Innovate, Mlandizi, Pwani, ambapo pia alishiriki uzinduzi wa mabweni ya shule hiyo na zoezi la upandaji miti.
Alisema malezi ya mtoto si jukumu la shule pekee, bali yanahitaji ushirikiano kati ya wazazi, walimu na walezi, hususani katika kufuatilia maendeleo ya kielimu, kitabia na kimaadili.
Lazima kuwe na ushirikiano kati ya wazazi, walimu na walezi. Hatuwezi kuwaachia walimu jukumu lote la kulea watoto, kwa sababu ili tupate viongozi bora wa taifa, kila upande lazima utekeleze wajibu wake,
Aidha, Msakulo alishiriki kupanda mti kama sehemu ya kuhamasisha wanafunzi na jamii kwa ujumla kutunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shule ya Innovate, George Ndaki, alisema shule hiyo hailengi kutoa elimu ya darasani pekee, bali kuwajengea wanafunzi uwezo wa kutumia maarifa wanayopata katika mazingira halisi.
Alisema shule hiyo pia inaweka mkazo katika sayansi na teknolojia ili kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na mahitaji ya dunia ya sasa.
Aliongeza kuwa uzinduzi wa mabweni ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na malezi ya wanafunzi, alisema mazingira bora yanachangia kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.







Post A Comment: