Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, ameipongeza Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) kwa kazi kubwa inayoendelea kuifanya katika kuimarisha huduma za kijamii zenye lengo la kukuza ustawi wa jamii.

Pongezi hizo amezitoa alipokutana na Kamati ya Maandalizi ya Kambi ya Sita ya Afya Bora, Maisha Bora ofisini kwake Vuga.

Kikao hicho kililenga kumpa taarifa kuhusu maandalizi ya Kambi ya Matibabu Bure itakayofanyika Kinduni, Unguja, kuanzia tarehe 3 hadi 7 Novemba 2026.

Mhe. Hemed ameipongeza ZMBF kwa jitihada zake za kumsaidia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuwaletea wananchi maendeleo. Amesema malengo ya taasisi hiyo yanajieleza wazi, kwani yanalenga kutatua changamoto zinazogusa maisha ya wananchi.

Ameahidi kuwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais itaendelea kushirikiana kikamilifu na ZMBF pamoja na Wizara ya Afya ili kufanikisha kambi hizi muhimu kwa jamii.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa ZMBF, Bi. Rehema Tukai, amesema taasisi hiyo inaendelea na kampeni ya Afya Bora, Maisha Bora, yenye lengo la kutambua na kutatua changamoto za kiafya zinazowakabili wananchi wa Zanzibar.

Amesema kambi zilizopita zimepokelewa kwa hamasa kubwa, huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kupata uchunguzi wa afya na matibabu mbalimbali. Hadi kufikia kambi nne za mwanzo, zaidi ya wanufaika 30,000 wa Unguja na Pemba walikuwa wamehudumiwa.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: