Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Makamba amesema wananchi wanaoishi katika maeneo ya mijini yenye sura ya vijijini watanufaika na huduma ya umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), hatua inayolenga kuwawezesha wananchi wenye kipato cha chini kupata huduma hiyo kwa gharama nafuu.
Akizungumza leo Octoba 16, 2026 jijini Mbeya, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, Mhe. Salome amesema Serikali imefanyia kazi maelekezo kuhusu utaratibu huo, ambapo maeneo husika tayari yametambuliwa na hatua za awali za manunuzi ya vifaa zinaendelea.
Amesema utaratibu huo unalenga kuhakikisha wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo kisheria ni ya mijini lakini yana hali inayofanana na vijijini wanapata fursa ya kuunganishiwa umeme kwa gharama nafuu, kwa kuzingatia hali zao za kiuchumi.
Aidha, ameeleza kuwa kwa wananchi wa mijini ambao hawana uwezo wa kulipa gharama za kuunganishiwa umeme za shilingi 320,000 kwa mara moja, Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, imezindua mfumo unaomwezesha mteja kuunganishiwa umeme kwanza na kulipa gharama hizo kidogokidogo kulingana na matumizi yake ya umeme.
Mhe.Salome amesisitiza kuwa, hatua hizo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kurahisisha upatikanaji wa huduma ya umeme kwa wananchi wa makundi mbalimbali, kwa lengo la kuongeza matumizi ya umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo ya jamii nchini.











Post A Comment: