MFANYABIASHARA Dennis Steven maarufu King Papaa ametoa msaada wa tani 1.4 za mchele na tani 1.4 za unga kwa mashehe, walimu wa madrasa na viongozi wasaidizi wa misikiti katika Kata ya Kimara, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya sadaka na jitihada zake za kusaidia jamii.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo, King Papaa alisema ameamua kutoa chakula hicho ili kusaidia viongozi hao wa dini pamoja na jamii kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.

“Nimeona sadaka yangu pia iwe sehemu ya chakula,” alisema King Papaa.

Alisema uamuzi wa kuwasaidia viongozi hao umetokana na mchango wao katika kueneza mafundisho ya dini, kuelimisha waumini na kujenga jamii yenye maadili.

King Papaa pia aliwataka wafanyabiashara, viongozi wa Serikali, wabunge na madiwani kutumia sehemu ya walichojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwasaidia wananchi, badala ya kuwasaidia wakati wa kampeni pekee.

Aidha, aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuwaelimisha waumini kuhusu tahadhari zinazotolewa na Serikali kuhusu mvua za El Niño, akisema misikiti na maeneo mengine ya ibada ni sehemu muhimu ya kuwafikia wananchi kwa ujumbe mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa BAKWATA Kata ya Kimara, Khamis Rashid, alimpongeza King Papaa kwa msaada huo, akisema umeonyesha huruma na kujali jamii.

Rashid aliwataka watu wenye uwezo kuiga mfano huo kwa kutumia sehemu ya walichonacho kuwasaidia wananchi wenye mahitaji.

Naye mkazi wa Kimara, Abdull Aziz, alisema King Papaa amekuwa akitoa misaada katika eneo hilo mara kadhaa, akieleza kuwa tayari amefanya hivyo zaidi ya mara tatu au nne.

Alisema mfanyabiashara huyo amekuwa mfano kwa vijana kutokana na kujitolea kwake kusaidia jamii, akitolea mfano tukio la kumchangia mama mmoja Sh500,000 kwa ajili ya kuwasaidia watoto wake kupata sare za shule.

Abdull alisema misaada hiyo inaonyesha umuhimu wa watu wenye uwezo kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: