Na: Chedaiwe Msuya, WF – Kampala
Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) imeendelea kuongeza fursa za uwekezaji na ufadhili wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu katika nchi wanachama.
Mchango huo umeendelea kuonekana kupitia ufadhili na uwekezaji wa Benki katika sekta mbalimbali, ikiwemo miundombinu, makazi, huduma za kifedha, viwanda na huduma za kijamii.
Katika taarifa iliyotolewa katika Mkutano wa Baraza la Uongozi la Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), uliofanyika Jijini Kampala, Uganda, pamoja na mambo mengine, Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Benki hiyo walijadili na kupitisha maazimio mbalimbali yanayolenga kuimarisha utendaji wa Benki, kuongeza uwezo wa kutoa huduma za kifedha na kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu katika nchi wanachama,ambapo, Tanzania katika mkutano huo iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ambaye ni mjumbe wa Baraza la Uongozi la EADB.
Katika taarifa hiyo ilionesha kuwa Tanzania imeendelea kunufaika na ufadhili wa miradi mbalimbali kutoka EADB ikiwemo ufadhili wa mradi wa Reli ya kisasa ya SGR (Lot 3 na 4) ambao unajumuisha ujenzi wa reli yenye urefu wa kilometa 294 kutoka Makutopora hadi Tabora na kipande cha kilometa 130 kutoka Tabora hadi Isaka.
Uwekezaji katika miundombinu ya kimkakati kama SGR una mchango mkubwa katika kuimarisha usafirishaji wa abiria na mizigo, kurahisisha shughuli za biashara na kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko.
Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na EADB umekuwa na umuhimu mkubwa katika kukuza sekta za uzalishaji, hususan kilimo, viwanda na biashara, kupitia Taasisi za fedha za ndani zinazoshirikiana na EADB zikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB); Azania Bank PLC na TIB Development Bank, ambazo zimekuwa zikitoa fursa za upatikanaji wa fedha kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji, hivyo kusaidia wafanyabiashara, wazalishaji na wawekezaji kupanua shughuli zao na kuongeza mchango wao katika uchumi.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unaendelea kuimarisha nafasi ya nchi katika ushirikiano wa kikanda na kuongeza fursa za kupata mitaji ya muda mrefu kwa ajili ya uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Baraza la Uongozi la EADB lilimteua Bi. Anne Juuko kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo kuanzia tarehe 2 Oktoba 2026, baada ya Uongozi wa kipindi cha mpito chini ya Mkurugenzi Mwandamizi wa Fedha na Hazina, Bw. Benard Mono. Kabla ya uteuzi huo Bi. Juuko aliwahi kuongoza sekta mbalimbali za fedha nchini Uganda ikiwemo Stanbic Bank Uganda na Global Markets – East Africa chini ya Standard Bank Group.
EADB ni Taasisi ya fedha ya Maendeleo ya Kikanda inayomilikiwa na nchi wanachama, zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda, pamoja na Taasisi nyingine za fedha na maendeleo ikilenga kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia utoaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika nchi wananchama.

Post A Comment: