
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Bw. Alban Mark Kihula, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Septemba 18, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.
Na Mwandishi Wetu - DODOMA
Wakala wa Vipimo Nchini (WMA), umeonya wafanyabiashara wanaotumia vipimo visivyo sahihi au kuuza bidhaa kwa vipimo visivyokidhi viwango kwamba wanakabiliwa na adhabu kali kwa mujibu wa sheria, ikiwemo faini na kifungo
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 18, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Mtumba jijini Dodoma, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Bw. Alban Kihulla, amesema mtuhumiwa anayekubali kosa anaweza kutozwa faini ya Shilingi 100,000 hadi 20,000,000 kwa kosa moja, huku anayekataa kosa na kupatikana na hatia anapelekwa Mahakamani na kutozwa faini ya Shilingi laki tatu hadi milioni 50, au faini na kifungo kisichozidi miaka miwili.
Amesema kwa mkosaji wa mara kwa mara, faini inaweza kuwa kati ya Shilingi 500,000 na milioni 100 kwa kosa moja, hatua inayolenga kuhakikisha wafanyabiashara wanazingatia matumizi ya vipimo sahihi na kulinda haki za walaji.
Bw. Kihulla amewataka wakulima kuachana na matumizi ya magunia, madebe, makopo, mafungu na vipimo vingine visivyo rasmi katika biashara ya mazao, akisisitiza matumizi ya mizani kwa kuwa kilo ndiyo kipimo kinachotambulika katika biashara kote duniani.
Amesema matumizi ya vipimo visivyo rasmi yanaweza kusababisha kutokuwepo kwa usawa katika biashara, hivyo wananchi wanapaswa kudai kupimiwa bidhaa kwa mizani ili kuhakikisha wanapata kiasi halisi wanacholipia.
“Madebe, makopo, visado na mafungu siyo vipimo, wafanyabiashara tumieni mizani,” amesisitiza Kihulla, akieleza kuwa WMA inahakikisha kilo moja inakuwa kilo moja na vipimo vyote vinazingatia viwango vinavyotambulika.
Aidha, amesema WMA haisimamii vipimo vya bidhaa pekee, bali inahakikisha usahihi wa vipimo katika sekta mbalimbali kwa mujibu wa sheria za kitaifa, kikanda na kimataifa.
Bw. Kihulla ametoa mfano wa sekta ya afya, ambako vipimo vya uzito vimekua vikihakikiwa ili kuhakikisha mgonjwa anapata uzito halisi, jambo linalomsaidia daktari kuamua kiwango sahihi cha dawa kinacholingana na uzito wa mgonjwa.
Amewataka wananchi kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya matumizi ya vipimo visivyo sahihi kwa kutoa taarifa wanapobaini au kuhisi kuwa vipimo vinavyotumika au walivyopimiwa si sahihi kwa kuwasiliana na WMA kupitia namba 08001197 ili kutoa taarifa na kupata msaada na kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa.



Post A Comment: