Kikosi kazi cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Vipimo (WMA) na Tume ya Ushindani (FCC), kimebaini kasoro mbalimbali katika bidhaa za pembejeo za kilimo, vipodozi, vifaa vya ujenzi na vyakula, baada ya kufanya ukaguzi wa siku tano mkoani Njombe.
Taasisi hizo zimesema ukaguzi na utoaji elimu kwa wafanyabiashara pamoja na wananchi utaendelea kufanyika mara kwa mara, kwa lengo la kumlinda mlaji na kuhakikisha bidhaa zinazouzwa zinakidhi viwango vya ubora na ujazo unaotakiwa.
Meneja wa TBS Kanda ya Mbeya, Rodney Alananga, amesema baadhi ya kasoro zilizobainika katika bidhaa hizo ni ukiukwaji wa sheria na taratibu zinazohusika.
Kaimu Meneja wa WMA Mkoa wa Njombe, Shabani Kingu, amesema miongoni mwa changamoto zilizobainika ni kuwepo kwa mifuko ya mbolea yenye ujazo pungufu.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa FCC Kanda ya Mbeya, Anderson Lwiza, amesema baadhi ya wafanyabiashara waliobainika kutumia au kunakili nembo za bidhaa za wazalishaji wengine wamechukuliwa hatua za kisheria.
Amesema hatua hizo zinalenga kuwalinda wazalishaji halali dhidi ya ushindani usio wa haki na kuhakikisha watumiaji wanapata bidhaa halali na salama.
Mfanyabiashara wa vipodozi mjini Njombe, Neema Michael, amesema ukaguzi unaofanywa na TBS umekuwa na mchango katika kuboresha biashara zao na kulinda afya za watumiaji.
Naye mkufunzi, Lameck Mgaya, amezitaka taasisi hizo kuongeza ukaguzi wa mara kwa mara, hususan katika bidhaa za pembejeo za kilimo, ili kuhakikisha bidhaa zinazowafikia wananchi zinakuwa na ubora na ujazo unaostahili.













Post A Comment: