Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steven Mengele almaarufu Steven Nyerere, amekosoa vikali tabia ya baadhi ya wanajamii kuwa na mtazamo hasi dhidi ya viongozi na watu maarufu wanaopata mafanikio katika maisha.

Akizungumza leo katika Ofisi za Taasisi hiyo, Steve Nyerere, ambaye pia ni kada wa siasa na msanii mkongwe wa filamu nchini, amesema anakerwa na dhana inayoanza kujengeka miongoni mwa baadhi ya watu kwamba kiongozi au mtu maarufu anayefanikiwa kimaisha amefikia hatua hiyo kutokana na wizi, ufisadi au kuingia mikataba isiyo halali.

Amesema mtazamo huo si wa kujenga kwa kuwa unaweza kuwakatisha tamaa viongozi, vijana na watu wengine wenye nia ya kufanya kazi kwa bidii, kutumia maarifa na ubunifu ili kujikwamua kiuchumi.

“Si kila mtu anayefanikiwa ameiba au amefanya ufisadi. Kuna watu wanafanya kazi kwa bidii, wana maarifa na wanatumia fursa zilizopo. Tujifunze kuheshimu mafanikio ya wengine,” amesema.

Ametoa wito kwa wananchi kuacha kuwahukumu watu kwa hisia au dhana zisizo na ushahidi, badala yake kujenga utamaduni wa kuthamini juhudi, ubunifu na hatua za kimaendeleo zinazofanywa na watu wengine.

Amesema Tanzania inapaswa kuendelea kujenga mazingira yatakayowezesha kuibuka kwa matajiri wengi wazawa, akisisitiza kuwa jamii haipaswi kuwakatisha tamaa watu wanaopiga hatua kiuchumi kwa kuwahusisha na tuhuma za wizi au ufisadi bila kuwa na ushahidi.

“Lazima nchi kama nchi iendelee kutengeneza matajiri wazawa wengi. Tusiwatishe na kuwakatisha tamaa kwa kuwahusisha na tuhuma za wizi na ufisadi bila kuwa na ushahidi wowote,” amesema.

Steve Nyerere amesema kuwa jamii inapaswa kuwa chanzo cha hamasa kwa vijana na watu wanaotafuta mafanikio, badala ya kuwakatisha tamaa, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu mafanikio ya wengine na kujifunza kutoka kwa watu waliofanikiwa.



Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: