Na Denis Chambi, Tanga
SERIKALI ya mkoa wa Tanga imewaagiza wamiliki wote wa Mabasi yanayosafirisha abiria kwenda nje ya mkoa huo na maeneo mbalimbali ya nchi kuhakikisha kuwa ifikapo September 8,2026 Magari yote yanaanza na kumaliza safari zake katika kituo kikuu cha Mabasi kilichopo Kange.
Agizo hilo linatokana na maadhimio yaliyotolewa na ofisi ya Waziri mkuu, Kamati ya Bunge inayoshughulika na Ofisi ya Rais tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa 'TAMISEMI' pamoja na wamiliki na wadau wa usafirishaji kwa lengo la kuhakikisha huduma ya usafirishaji inaimarika pamoja na kuchangia maendeleo ya mkoa huo hususani kwa kwa Halmashauri ya jiji la Tanga kupitia kituo hicho ambacho kinatarajia kuwa kitomvu cha uchumi kwa wananchi .
Akizungumza katika kikao cha pamoja na wadau wa usafirishaji wakiwemo wamiliki wa Mabasi, Baraza la madiwani na ofisi ya halmashauri ya jiji la Tanga Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani amesema kuwa utekelezaji wa agizo hilo umezingatia utekelezaji wa Sheria ndogo ya Halmashauri 'by laws' ya mwaka 2019 huku akiitaka Halmashauri kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau wote wa usafirishaji.
"Baada ya kupitia mapendekezo na ushauri ulioyotolewa na wadau wa usafirishaji na viongozi mbalimbali kwa kuzingatia Sheria ndogo ya Halmashauri 'by laws' ya mwaka 2019 Magari yote yatapaswa kuanza na kumaliza safari zake katika kituo kikuu cha Mabasi Kange wamiliki wote wanapaswa kuzingatia Sheria hizi na tumekubaliana suala hili lianze rasmi tarehe 8,2026" amesema Dkt Buriani.
Amesema kuwa agizo hilo limeambatana na mapendekezo ambayo yanatakiwa kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kuitaka mamlaka ya udhibiti wa usafiri ardhini 'LATRA' kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za vijijini na mijini kuanzisha njia za safari za Daladala zinazotoka maeneo mbalimbali ya jiji kwenda katika kituo hicho cha Kange, kuwepo kwa gari la Zimamoto na uokoaji, kukaguliwa kwa vituo vyote vya Mabasi vilivyopo katikati ya jiji kama vinakidhi vigezo.
Aidha kabla ya kutekelezwa kwa agizo hilo Balozi Dkt. Buriani ameiagiza Halmashauri ya jiji la Tanga kuhakikisha kuwa katika kituo hicho kunakuwa na maeneo maalumu kwaajili ya maegesho la Daladala, Bodaboda, Magari binafsi na kuweka mabango ili kuwarahisishia abiria na wananchi kuweza kuendelea na safari zao.
Amewataka wamiliki wote wa Mabasi mkoani humo kuhakikisha wanakuwa na maeneo maalumu kwaajili ya kupaki Magari yao ambayo yatakuwa yakisubiri safari tofauti na sasa ambapo baadhi yao hutumia barabara zilizopo katikati ya jiji hilo na kusababisha msongamano.
"Wale wenye terminal zao huko itabidi sasa terminal hii ya Kange iwe ndio inafanya kazi lakini hatuwakatazi kuwa na terminal zenu hiyo lazima iwe imezungushiwa ukuta ambapo gari linaweza kwenda kufanyiwa marekebisho wakati likisubiri safari" amesisitiza Dkt Buriani.
Akizungumza katika kikao hicho Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya jiji la Tanga Khalid Hamza amepongeza maadhimio hayo na kuahidi kuendelea kusimamia uboreshaji wa kituo hicho ambacho mbali na kuwa kituo kikuu cha Mabasi kinatarajia kuwa kitomvu cha uchumi kwa wananchi na Serikali kuendelea kukusanya mapato.
"Tunaendelea kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani kwa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inaletwa katika mkoa wetu hususani jiji letu la Tanga sisi kama halmashauri tuko tayari kupokea maelekezo na kwenda kuyafanyia kazi kuhakikisha stendi yetu inafanya kazi kwaajili ya mapato ya Halmashauri yetu" amesema Hamza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama Cha wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Abdi Awadhi amepongeza kutekelezwa kwa baadhi ya mapendekezo ambayo waliyatoa hapo awali huku akiiomba Serikali Mabasi yote kuendelea kushusha na kupakia abiria wake nyakati za usiku katika terminal zao za siku zote wakati ambapo bado miundombinu inaendelea kuboreshwa katika kituo hicho cha Kange.
"TABOA mkoa wa Tanga tumeridhia maelekezo yote ambayo umeyatoa mkuu wa mkoa na kamati uliyoiunda kwaajili ya maboresho ya mpito yaliyotolea sisi tunaomba turuhusiwe kushusha na kupakia abiria Tanga mjini nyakati za usiku kutokana na kituo chetu hali ya usalama bado hijakuwa sawa" amesema Awadhi.
Kikao hicho pia kimeadhimia kuwa mara tu baada ya kuanza kutekelezwa kwa agizo hilo wadau wote wa usafirishaji, wamiliki wa Mabasi pamoja na Serikali kila baada ya mwezi kuweza kukutana kufanya tathmini ya mkakati huo na kufanyika kazi mapungufu ambayo yanatakiwa kuboreshwa ili kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi.


Post A Comment: