Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na usimamizi wa rasilimali madini, kwa lengo la kuhakikisha utajiri wa madini unatumika kikamilifu katika kujenga uchumi wa taifa na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.

Prof. Shemdoe amesema hayo Septemba 16, 2026, akiwa Ruangwa mkoani Lindi, wakati akifungua Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji mkoani humo.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa sekta ya madini haibaki kuwa ya uchimbaji pekee, bali inakuwa kichocheo cha viwanda, teknolojia, ajira, biashara, ubunifu na maendeleo ya jamii,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Katika kuhakikisha lengo hilo linatimia, Prof. Shemdoe ameyataka makampuni makubwa yaliyowekeza katika sekta ya madini kuangalia namna bora ya kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji wa madini mkoani Lindi, hususan katika maeneo yenye rasilimali hizo, ili wananchi wanaozunguka maeneo hayo wanufaike zaidi kupitia fursa za ajira.

Prof. Shemdoe amesema maonesho hayo ni jukwaa muhimu linalowaunganisha Serikali, wananchi, wawekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi, wataalam pamoja na taasisi za kifedha, kwa ajili ya kujenga uelewa mpana kuhusu rasilimali zilizopo na fursa za uwekezaji, pamoja na namna sekta mbalimbali za uchumi, ikiwemo madini, zinavyoweza kuongeza ajira, mapato na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Nilipofika hapa nilitembelea mabanda mbalimbali yaliyowakutanisha wachimbaji wakubwa, wadogo, wanaoleta teknolojia, akina mama, vijana na taasisi za kifedha, ili wakitoka hapa watoke na fursa mbalimbali zinazotokana na uwekezaji katika sekta ya madini,” ameeleza Prof. Shemdoe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Adam Kighoma Malima, amesema mkoa huo si maskini, bali changamoto ni wananchi wake kuwa maskini, kwani mkoa hauwezi kuitwa maskini wakati una utajiri wa madini mbalimbali, jambo aliloliona kupitia maonesho hayo.

Mhe. Malima ameahidi kuwa ofisi yake itaendelea kusimamia maonesho kama hayo ya madini ili yaendelee kuibua fursa na kuvutia uwekezaji utakaowanufaisha wananchi.

Aidha, Mhe. Malima amesema anatarajia kuwa ndani ya kipindi cha uongozi wa miaka mitano wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoa wa Lindi utakuwa umetambua fursa zake, kuzipa kipaumbele na hatimaye kuwa miongoni mwa mikoa yenye mapato makubwa nchini.

Naye Mbunge wa Ruangwa ambaye pia ni Naibu Waziri, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amesema Ruangwa ina kiwanda kikubwa cha graphite, huku akieleza kuwa madini yaliyopo wilayani humo si graphite, dhahabu na kopa pekee, bali yapo madini mengine mengi.

Mhe. Mmuya amesema kutokana na uwepo wa rasilimali hizo, Ruangwa imeendelea kunufaika na mapato yatokanayo na sekta ya madini, ambapo mwaka jana wilaya hiyo ilichangia kiasi cha shilingi bilioni 2.9.














Share To:

Post A Comment: