Na: OWM – TAMISEMI, Ruangwa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kukamilisha mchakato wa kushughulikia upatikanaji wa hati ya umiliki wa ardhi kwa ajili ya Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mkoani Lindi.

Prof. Shemdoe ametoa agizo hilo wakati wa kikao kazi chake na viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi na Chuo Kikuu cha Dar es salaaam (UDSM), kilicholenga kupata ufumbuzi wa changamoto zinazohusu maendeleo ya kampasi hiyo, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Lameck Mwigulu Nchemba alilolitoa wakati wa ziara yake mkoani Lindi akielekeza hatua zichukuliwe kuhakikisha kampasi hiyo ya UDSM Lindi inapata hati ya umiliki wa ardhi.

Katika kikao hicho kilichofanyika Septemba 16, 2026 Ruangwa mkoani Lindi, Prof. Shemdoe amemsisitiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Bw. Juma Mnwele, kuhakikisha suala la hati ya umiliki wa ardhi la Kampasi hiyo ya UDSM Lindi linashughulikiwa kwa haraka na apatiwe mrejesho wa utekelezaji wake.

Aidha, Prof. Shemdoe ameiagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Lindi kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 1.5, itakayounganisha Kampasi hiyo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Lindi na barabara kuu ya Lindi.

Kikao hicho cha Prof. Shemdoe kwa upande wa Serikali kilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Adam Kighoma Malima, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya,    Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Bw. Juma Mnwele, Meneja wa TARURA Mkoa wa Lindi Mhandisi Alberto Kindole, pamoja wataalam na viongozi wengine wa Mkoa.

Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), kikao kazi hicho kiliudhuriwa na ujumbe uliongozwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala (DVC-PFA), Prof. Bernadeta Killian.












Share To:

Post A Comment: