Na, Denis Chambi Tanga.
UKOSEFU wa elimu sahihi ya matumizi ya dawa pamoja na hali duni ya kimaisha kwa waraibu wa madawa ya kulevya zimetajwa kuwa chanzo kikuu cha waraibu wengi kupoteza maisha hii ikichangiwa pia na wengi kuacha kutumia dawa ambazo zinaweza kuwasaidia kupata nafuu.
Hayo yamebainishwa na Katibu mtendaji kutoka Asasi ya Kiraia ya Gift of Hope Saidi Bandawe wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisni kwake akieleza kuwa waraibu 94 kati ya 1537 waliokiwa wakipatiwa dawa katika kituo cha Methadone kilichopo katika Hospital ya rufaa Bombo wamefariki Dunia.
" Kuna changamoto imejitokeza kwa waraibu kuzidisha kiwango cha dawa wanazotakiwa kutumia wengi wanapoteza maisha bado tunaendelea kutoa elimu kwa jamii na wananchi uelewa sahihi wa matumizi au madhara yatokanayo na dawa za kulevya, kuzidisha kiwango cha dawa na hii imeonyesha kwa mkoa wa Tanga kupitia kituo Cha methadone kuna watu 94 wamepoteza maisha"
Amesema kupitia elimu mbalimbali wanayoendelea kuitoa kwa jamii juu ya athari za madawa ya kulevya matumizi ya dawa aina ya Heroine yamepungua kwa kiasi kikubwa ikikadiriwa kufikia asilimia 99.
Aidha mratibu huyo ameipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya kudhibiti dawa za kulevya nchini kwa jitihada mbalimbali zinazofanyika za kudhibiti na kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya ambapo mbali na kituo Cha Methadone kilichopo Hospital ya rufaa Bombo kimejengwa kituo kingine kilichopo Wilayani Muheza.
"Tunaipongeza na kuishukuru Serikali yetu kupitia Mamlaka ya kudhibiti dawa za kulevya nchini matumizi ya madawa ya kulevya yamepungua kwa kiasi kikubwa na hii ni faida kwa sababu matukio ya kiuhalifu yatapungua katika jamii zetu"
Bandawe amezitaja sababu za kuwepo kwa waraibu wa madawa katika jamii ambapo amesema kuwa upatikanaji kirahisi wa dawa hizo ikiwemo,Bangi Mirungi, Pombe , makundi rika, pamoja na ukosefu wa elimu.
Amebainisha kuwa kitakwimu wilaya 5 kati ya 9 zilizopo mkoani Tanga zimekuwa na waathirika wengi wa dawa za kulevya ambazo ni Korogwe, Tanga mjini, Muheza, Mkinga pamoja na Handeni huku akitaja mafanikio waliyoyapata tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo ambapo wameweza kuwasajili watu zaidi ya 576 kwenye kupata tiba nafuu.



Post A Comment: