Na Shua Ndereka, Morogoro
Serikali mkoani Morogoro imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na migogoro ya wakulima na wafugaji, huku Mkuu wa Mkoa huo, Queen Sendiga, akitangaza kipindi cha siku 60 cha kushughulikia changamoto hiyo na kutafuta suluhisho la kudumu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Sendiga amesema katika kipindi hicho Serikali itafanya utambuzi wa maeneo yenye migogoro, kusikiliza pande zote zinazohusika na kuhakikisha maamuzi yatakayofikiwa kwa lengo la kuleta amani na usalama yanatekelezwa.
Amesema moja ya hatua zitakazochukuliwa ni kufanya zoezi la utambuzi wa mifugo yote iliyopo mkoani humo, hatua inayolenga kupata takwimu sahihi kuhusu idadi ya mifugo, maeneo inayotumia pamoja na kusaidia katika kupanga matumizi bora ya ardhi.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, zoezi hilo linatarajiwa kuanza Septemba 18, 2026, na litaendelea kwa siku 60 huku Serikali imejipanga kuhakikisha migogoro ya wakulima na wafugaji inapata suluhisho la kudumu kwa kuzingatia kanuni na sheria zilizopo.
“Serikali mkoani Morogoro haitasita kumchukulia hatua mfugaji yeyote anayevunja sheria mahali popote, ikiwa ni pamoja na kuhuisha kamati za amani na usalama katika kata na mabaraza ya kutatua migogoro kwenye kata kama ilivyokuwa zamani,” amesema Sendiga.
Aidha, amesema viongozi watakaobainika kutumia nafasi zao kuchochea migogoro kati ya wakulima na wafugaji watachukuliwa hatua kali, akieleza kuwa vitendo hivyo vinaweza kuhatarisha amani na kuvuruga shughuli za uzalishaji.
Amewataka wananchi kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa sahihi na kufuata taratibu zilizowekwa katika utatuzi wa migogoro, badala ya kuchukua sheria mkononi.




Post A Comment: