Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imejipanga kikamilifu kuhakikisha inatoa huduma za matibabu na tiba za kibobezi kwa wanamichezo watakaoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuelekea mashindano hayo makubwa ya kimataifa.


MOI imesema imeweka mikakati mahsusi ya kuhakikisha wanamichezo watakaopata changamoto za majeraha wakati wa michuano hiyo, pamoja na wale watakaohitaji kupima afya zao, wanapata huduma za kisasa, za haraka na zenye viwango vya kimataifa.

Akizungumza leo jijini Dodoma kuhusu maandalizi hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema taasisi hiyo iko tayari kutumia wataalamu, miundombinu na teknolojia ilizonazo kuhakikisha wanamichezo wanapata huduma bora wakati wote wa michuano.

Amesema MOI ina zaidi ya Madaktari Bingwa Bobezi sita (6) waliobobea katika tiba za michezo (Sports Medicine), ambao wamepata mafunzo katika mataifa mbalimbali duniani na kurejea nchini wakiwa na ujuzi na uzoefu unaowawezesha kutoa huduma maalum kwa wanamichezo.

Kwa mujibu wa Dkt. Ulisubisya, baadhi ya wataalamu hao pia wamekuwa wakihudumia timu ya Taifa pamoja na kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), jambo linaloongeza uwezo wa MOI katika kushughulikia mahitaji ya kiafya ya wanamichezo wa ngazi ya juu.


KLINIKI MAALUM KWA WAGONJWA WA KIMATAIFA


Katika maandalizi hayo, MOI imeeleza kuwa ina Kliniki Maalum ya Wagonjwa wa Kimataifa (Premier and International Patient Services) inayolenga kutoa huduma kwa haraka na kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya wagonjwa na wageni wa kimataifa.

Huduma hiyo inatarajiwa kuwa sehemu muhimu katika kuwahudumia wanamichezo na wajumbe wa timu mbalimbali watakaohitaji huduma za kitabibu wakati wa michuano.

Aidha, MOI ina vyumba 25 vya kisasa vya kulaza wagonjwa wa kimataifa (Premier Wards), ambavyo vimeandaliwa kutoa mazingira bora ya malazi na matibabu kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za kiwango cha juu.


TEKNOLOJIA NA VIFAA VYA KISASA

Dkt. Ulisubisya amesema uwezo wa MOI pia unaimarishwa na uwepo wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi, tiba na upasuaji, vinavyowezesha wataalamu kutoa huduma za kibobezi kwa usahihi na kwa wakati.

Miongoni mwa vifaa hivyo ni MRI, CT Scan, Cathlab, Arthroscopic Towers, Brain Lab, Digital X-Ray, Ultrasound za kisasa, vifaa vya kisasa vya Microscopy kwa ajili ya upasuaji wa ubongo na mgongo, C-Arms pamoja na ETV Towers, sambamba na vifaa vingine vya kisasa.

Kwa kuwa michezo ya ushindani inaweza kuhusisha majeraha ya aina mbalimbali, MOI imesema uwepo wa teknolojia hizo unaipa uwezo wa kufanya uchunguzi wa haraka na kutoa matibabu yanayohitajika kulingana na aina na ukubwa wa jeraha.


KITENGO CHA DHARURA CHAWEKWA TAYARI


MOI pia imeweka mkazo katika maandalizi ya Kitengo cha Dharura, ambacho kimeandaliwa mahsusi kuhakikisha kinakuwa tayari kutoa huduma wakati wa kipindi cha michuano.

Dkt. Ulisubisya amesema MOI tayari ina uzoefu wa kuandaa huduma za dharura wakati wa mashindano makubwa ya michezo, akitoa mfano wa michuano ya CHAN, ambapo taasisi hiyo ilishiriki katika kutoa huduma za afya kwa maandalizi maalum.

Amesema uzoefu huo umejenga uwezo na utayari wa taasisi hiyo kukabiliana na mahitaji ya kitabibu yatakayojitokeza wakati wa AFCON 2027.

Kwa ujumla, MOI imesisitiza kuwa imejipanga kutumia wataalamu wake, huduma maalum, miundombinu na teknolojia ya kisasa kuhakikisha Tanzania inakuwa na mfumo madhubuti wa huduma za afya kwa wanamichezo wakati wa AFCON 2027.

“MOI tuko tayari kwa michuano ya AFCON Zanzibar na mikoa ya Arusha na Dar es Salaam,” amesema Dkt. Ulisubisya.

Kauli hiyo inaweka wazi dhamira ya MOI kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya Tanzania katika kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa maandalizi ya kutosha, ikiwemo uwepo wa huduma za afya zinazoweza kukidhi mahitaji ya wanamichezo wa ndani na wa kimataifa.

Taarifa hiyo imetolewa wakati wa kuwasilishwa kwa Taarifa ya Mafanikio ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Julai 2025 hadi Juni 2026, iliyotolewa jijini Dodoma, Septemba 1, 2026, na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya.

Share To:

Post A Comment: