Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, amefungua Kliniki ya Ardhi katika Wilaya ya Muheza, akisisitiza umuhimu wa uratibu, mipango bora na ushirikishwaji wa wananchi katika matumizi ya ardhi.


Dkt. Burian amesema urasimishaji wa ardhi unapaswa kwenda sambamba na mipango shirikishi inayozingatia mahitaji ya wananchi, wawekezaji na maendeleo ya maeneo husika, huku akitaka taasisi za Serikali kufanya kazi kwa pamoja katika kupanga matumizi ya ardhi.



Amesema ni muhimu kuwa na ramani na mipango inayoainisha maeneo kwa matumizi mbalimbali, ikiwemo makazi, viwanda vikubwa na vidogo, barabara, ICD, hoteli, vituo vya elimu na maeneo ya biashara.


“Tunapofanya urasimishaji wa ardhi na kutenga maeneo, lazima kuwe na uratibu mzuri na wananchi washirikishwe katika kupanga matumizi ya maeneo yao,” amesema Dkt. Burian.

Amesema maeneo ya viwanda yanapaswa kutengwa kwa kuzingatia aina ya shughuli zinazofanyika ili kuepusha viwanda kujengwa katikati ya makazi na kusababisha changamoto kwa wananchi na wawekezaji.


“Tupange vizuri leo ili tuepuke migogoro na gharama kubwa kesho,” amesema.

Aidha, amesema pale wananchi wanapoathiriwa na upanuzi wa barabara au utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Serikali inapaswa kuhakikisha taratibu za fidia zinafuatwa na wananchi wanalipwa kwa wakati kwa mujibu wa sheria.


Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tanga, Jabir Singano, amesema Kliniki ya Ardhi inalenga kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kuwawezesha kupata huduma mbalimbali katika eneo moja.


Singano amesema Kliniki hiyo ni sehemu ya mpango wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa kuwafikishia wananchi huduma, elimu na ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya ardhi.


Amesema kwa mwaka huu wa fedha, Kliniki za Ardhi zimepangwa kufanyika nchini kuanzia Septemba 22 hadi Oktoba 3, huku Mkoa wa Tanga ukianza Wilaya ya Muheza kuanzia Septemba 23 hadi Septemba 26, na baadaye Jiji la Tanga kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 3.


“Kwa siku ya kwanza tumeweza kusajili wananchi 110 na kutoa hati 50. Hadi leo, tayari tumeshasajili wananchi 104 na hati 21 zimeshachapishwa,” amesema Singano.


Ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa hiyo kupata huduma, elimu na ufafanuzi wa masuala ya ardhi, ikiwemo kutatua changamoto zinazohusiana na umiliki, matumizi na upatikanaji wa hati.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: