Kampuni ya JETOUR Tanzania imezindua JETOUR Club na kutambulisha magari mawili mapya yenye teknolojia ya plug-in hybrid, JETOUR G700 na JETOUR F700, hatua inayolenga kuwapa Watanzania chaguo zaidi katika matumizi ya usafiri unaozingatia ufanisi wa nishati.
Uzinduzi huo unafanyika wakati dunia ikikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mafuta na kuongezeka kwa gharama za nishati, hali inayosukuma matumizi ya teknolojia zinazolenga kupunguza utegemezi wa mafuta.Tanzania nayo inaendelea kuchukua hatua katika kuhamasisha matumizi yenye ufanisi ya nishati na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya mafuta, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa JETOUR Tanzania, magari hayo mapya yanachanganya matumizi ya umeme na mafuta, hivyo kumpa mtumiaji fursa ya kutumia umeme katika safari fupi na mafuta kwa safari ndefu, kulingana na mahitaji ya safari.
Hatua hiyo inalenga kuongeza chaguo kwa Watanzania wanaohitaji magari yenye uwezo wa kufanya kazi katika mazingira mbalimbali, huku wakipata fursa ya kutumia teknolojia inayoweza kusaidia kupunguza matumizi ya mafuta ikilinganishwa na magari yanayotegemea mafuta pekee.
Uzinduzi huo umefanyika chini ya kaulimbiu “Africa Expedition 2025”, ikiwa ni sehemu ya mpango wa JETOUR Tanzania kwa kushirikiana na Africarriers Group wa kuimarisha uwepo wa chapa hiyo katika soko la Tanzania, sambamba na kuunganisha teknolojia ya magari ya kizazi kipya na uzoefu mpana wa umiliki.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JETOUR Tanzania, Zain Pirbhai, amesema kampuni hiyo inalenga kuwapatia wateja magari yanayokidhi mahitaji ya matumizi ya kila siku, safari za masafa marefu pamoja na shughuli za nje.
Amesema teknolojia ya plug-in hybrid inatoa unyumbufu zaidi katika matumizi ya nishati, kwa kumwezesha mtumiaji kutumia umeme na mafuta kulingana na aina na umbali wa safari.
“Tunataka kuwapa wateja wetu magari yanayokidhi mahitaji yao ya kila siku, safari ndefu na shughuli mbalimbali za nje, huku wakinufaika na teknolojia ya kisasa inayowapa unyumbufu katika matumizi ya nishati,” amesema Pirbhai.

.jpeg)


Post A Comment: