Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imetenga Shilingi bilioni 10 katika kipindi cha miaka miwili ya fedha, kuanzia mwaka 2025/2026 hadi 2026/2027, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa vya mafunzo ya amali katika shule mbalimbali za sekondari nchini.
Uwekezaji huo unalenga kuunga mkono utekelezaji wa mitaala inayowapatia wanafunzi maarifa, stadi na ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira, pamoja na kuwawezesha kutumia ujuzi wanaoupata shuleni katika kujiajiri na kuajiriwa.
Meneja wa Miradi ya Elimu wa TEA, Bi. Mwafatma Mohamed, amesema hayo wakati akieleza kuhusu mchango wa Mamlaka katika utekelezaji wa mitaala mipya mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, aliyetembelea banda la TEA katika Kongamano la Sita la Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika (African Curriculum Association–ACA) jijini Dar es Salaam.
Bi. Mohamed amesema TEA imeendelea kuweka kipaumbele katika uwekezaji wa miundombinu na vifaa vya mafunzo ya amali ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kupata stadi zinazohitajika katika maisha na soko la ajira.
“TEA imeendelea kutoa kipaumbele katika kuunga mkono utekelezaji wa mitaala mipya kupitia uwekezaji katika miundombinu na vifaa vya mafunzo ya amali. Katika kipindi cha miaka miwili ya fedha, tumetenga Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa vya mafunzo ya amali katika shule mbalimbali za sekondari nchini,” amesema.
Aidha, amesema TEA imetenga Shilingi bilioni 4.1 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi kupitia utekelezaji wa mpango wa Makundi Rika Mawili (Double Cohort).
Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za TEA katika kusaidia utekelezaji wa mitaala mipya kwa kuwawezesha wanafunzi kupata fursa za kujifunza kwa vitendo na kujenga uwezo wa kutumia maarifa na stadi wanazopata shuleni katika kujiajiri au kuajiriwa.
Katika ziara hiyo, Prof. Shemdoe, ambaye alikuwa mgeni wa heshima katika kongamano hilo, alitembelea banda la TEA na kupata maelezo kuhusu uwekezaji unaofanywa na Mamlaka katika kuboresha miundombinu na upatikanaji wa vifaa vya mafunzo ya amali.
Kongamano hilo la siku nne, lililoanza Septemba 22, 2026, limejikita katika kujadili mageuzi ya mifumo ya elimu barani Afrika, maboresho ya mitaala, maandalizi ya walimu na ubunifu jumuishi katika zama za Akili Unde (AI) na teknolojia zinazoibuka.
Kongamano hilo pia linawakutanisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali zinazohusika na uandaaji, uendelezaji na uboreshaji wa mitaala kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa lengo la kubadilishana maarifa, uzoefu na mbinu bunifu za kuimarisha mifumo ya elimu inayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Ushiriki wa TEA katika kongamano hilo unalenga pia kuchangia mijadala kuhusu namna uwekezaji katika miundombinu, vifaa na mazingira bora ya kujifunzia unavyoweza kusaidia utekelezaji wa mitaala inayozingatia maarifa na stadi zinazohitajika katika ulimwengu wa sasa, hususan kutokana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.














Post A Comment: