Na. Asia Singano na Josephine Majura, WF - Dodoma
Watumishi wa Wizara ya Fedha wanaotoa huduma kwa wananchi katika Maonesho ya 33 ya Kilimo ya Nanenane wamekumbushwa kuendelea kuzingatia weledi, uadilifu, uwajibikaji na maadili ya utumishi wa umma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, sahihi na zenye kuakisi dhamira ya Serikali ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.
Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Wizara ya Fedha, Bw. Simbani Liganga, wakati alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na taasisi zake katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.
Alisema Maonesho ya Nanenane ni jukwaa muhimu kwa Wizara ya Fedha, kuimarisha mawasiliano na wananchi kwa kuwapatia elimu kuhusu majukumu ya Wizara, Sera za Fedha, mchakato wa maandalizi na usimamizi wa bajeti ya Serikali, usimamizi wa mali za Serikali, pamoja na huduma nyingine zinazotekelezwa na taasisi zake na kuwakaribisha wananchi kutembelea Banda hilo.
‘’Naendelea kutoa wito kwa wananchi kuwa, Wizara ya Fedha, bado inaendelea kushiriki katika Maonesho mbalimbali ikiwemo haya ya Nanenane kwa hiyo nawaalika wananchi kushiriki na kuja kwenye Banda hili ili kupata huduma zote zinazotolewa na Wizara ya Fedha na watumishi wa Wizara waliopo hapa’’ alisema Bw. Simbani.
Alieleza kuwa ubora wa huduma zinazotolewa katika Maonesho hayo unachangia kujenga taswira chanya ya Wizara ya Fedha na Serikali kwa ujumla, hivyo amewataka watumishi kuwapokea wananchi kwa heshima, kuwahudumia kwa haraka, kusikiliza changamoto zao na kutoa majibu sahihi yanayozingatia taaluma, sheria na miongozo ya Serikali.
"Kila mwananchi anayefika katika Banda letu anapaswa kuondoka akiwa amepata elimu, ameridhishwa na huduma aliyopewa na ameongeza uelewa kuhusu mchango wa Wizara ya Fedha katika maendeleo ya uchumi wa Taifa, ili kuyafikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na hiyo ndiyo dhima ya ushiriki wetu katika Maonesho haya" alisisitiza Bw. Simbani.
Aliongeza kuwa ushiriki wa Wizara ya Fedha katika Maonesho mbalimbali ya kitaifa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwasogezea wananchi huduma, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara, pamoja na kujenga uelewa wa umma kuhusu sera na mipango ya maendeleo inayoratibiwa na wizara hiyo.
Wizara ya Fedha imeendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kutoa elimu ya fedha, kuhamasisha usimamizi mzuri wa rasilimali za umma na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wananchi, huku ikidhamiria kuendelea kushiriki maonesho mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, kutoa huduma zenye ubora na kuendelea kujenga jamii yenye uelewa mpana kuhusu masuala ya fedha na uchumi kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
.jpg)




.jpg)
Post A Comment: