Na OWM – TAMISEMI, Morogoro
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapongeza wakulima, wafugaji na wavuvi kwa mchango wao mkubwa uliowezesha Tanzania kufikia utoshelevu wa chakula wa zaidi ya asilimia 120, hatua inayodhihirisha mafanikio ya uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Dkt. Mwigulu aliwasilisha pongezi hizo za Mhe. Rais Agosti 4, 2026, alipotembelea Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika Viwanja vya Nane Nane mkoani Morogoro.
Katika ziara hiyo alijionea shughuli na ubunifu wa wakulima, wafugaji na wavuvi kutoka mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Pwani na Tanga.
Amesema maonesho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, "Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050," ambayo inawahimiza Watanzania kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji ya soko, kutumia teknolojia za kisasa, kuongeza ubora wa bidhaa na kuimarisha mnyororo wa thamani ili kufanya kilimo kuwa biashara yenye tija na mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
"Kwa nilichojionea kupitia maonesho ya mwaka huu, ninaziona dalili zote kwamba ifikapo mwaka 2050 malengo ya Dira ya Taifa tuliyojiwekea yatakuwa yamefikiwa, kwa kuwa tuko kwenye hatua nzuri ya utekelezaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi," amesema Dkt. Mwigulu.
Ameongeza kuwa ameridhishwa na ubora wa mazao mbalimbali yaliyooneshwa, ikiwemo nyanya, bilinganya na bidhaa nyingine zinazokidhi viwango vya masoko ya kimataifa, yakiwemo ya Marekani na Ulaya, jambo linaloashiria kuwa Tanzania ipo kwenye mwelekeo sahihi wa kuzalisha bidhaa zenye ushindani duniani.
Akizungumzia sekta ya mifugo na uvuvi, Dkt. Mwigulu amesema zimeendelea kuwa nguzo muhimu za uchumi wa taifa, akibainisha kuwa mchango wa sekta ya mifugo katika pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 2.3 hadi asilimia 6.2.
Ametoa mfano wa mafanikio ya wanaonufaika na sekta hiyo kwa kumtaja kijana mmoja mhitimu anayejihusisha na ufugaji wa kisasa, ambaye ameonesha ng'ombe mwenye uzito wa zaidi ya kilogramu 1,000 mwenye thamani ya takribani Shilingi Milioni 20. Aidha, amesema kijana huyo anafuga zaidi ya ng'ombe 200 na alipoulizwa na Waziri wa TAMISEMI kama anahitaji mkopo, alieleza kuwa hana uhitaji huo kutokana na mafanikio ya shughuli zake.
Awali, akitoa neno la utangulizi kabla ya Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi pamoja na washiriki wa maonesho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, alisema Waziri Mkuu alimpa jukumu la ulezi wa Mkoa wa Morogoro, hivyo alimkaribisha rasmi kama waziri mwenyeji wa mkoa huo, ambao ni mmoja wa mikoa inayounda Kanda ya Mashariki katika Maonesho ya Nane Nane.












Post A Comment: