
Kaswaga ameeleza kuwa e-GA imeendelea kupanua matumizi ya teknolojia kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, ambapo imejenga mfumo unaosaidia kuimarisha usimamizi wa vyama vya ushirika. Kupitia mfumo huo, wakulima wana uwezo wa kufuatilia masoko ya mazao, mwenendo wa mauzo na kupata taarifa muhimu zinazowawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kibiashara.
Katika kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, amesema e-GA imeungana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuanzisha Mfumo wa Usimamizi wa Mbolea (Fertilizer Information System – FIS), unaowezesha usajili wa wazalishaji, waagizaji na wasambazaji wa mbolea pamoja na ufuatiliaji wa bei elekezi ili kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kwa wakati na kwa gharama zinazokubalika.
Aidha, amesema e-GA inaendelea kuunganisha mifumo ya taasisi mbalimbali za Serikali, hatua ambayo imepunguza urasimu, kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Hata hivyo amewataka wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nane Nane kutembelea banda la e-GA ili kupata elimu kuhusu huduma mbalimbali za Serikali zinazopatikana kidijitali na kujionea namna teknolojia inavyochangia kuimarisha uzalishaji wa kilimo na maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Post A Comment: