
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mkutano mkuu wa wanahisa wa Afrika50 na jukwaa la miundombinu Afrika, Agosti 03, 2026, Ofisi za Wizara ya Fedha, jijini Dar es salaam.
TANZANIA itakuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 (Africa50 General Shareholders' Meeting - GSM) pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), yatakayofanyika Agosti 5 na 6, 2026 katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), Dar es Salaam.
Na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mwenyeji na mwenyekiti wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huo, ambao pia utahusisha taasisi mbalimbali za umma na sekta binafsi nchini, benki za biashara na maendeleo, taasisi za hifadhi ya jamii, masoko ya mitaji na wadau wa sekta za nishati, uchukuzi, reli, bandari, usafiri wa anga, maji, afya, madini, mafuta na gesi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo Septemba 03, 2026 Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema mkutano huo wa kimataifa unafanyika wakati Africa50 inatimiza miaka 10 tangu kuanza shughuli zake mwaka 2016, huku ukitarajiwa kukutanisha washiriki zaidi ya 1,200 kutoka Afrika na maeneo mbalimbali duniani.
Balozi Omar amesema Africa50 ilianzishwa mwaka 2013 kwa ushirikiano wa Serikali za Afrika na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ikiwa na lengo la kuharakisha maandalizi, uendelezaji na ufadhili wa miradi mikubwa ya kimkakati ya miundombinu kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi katika sekta za nishati, uchukuzi, afya, elimu, TEHAMA na huduma za kifedha.
Amesema Tanzania ilijiunga rasmi na Africa50 Februari 14, 2023 kama mwanahisa wa kundi la “A” (African Sovereign States), hatua iliyopanua fursa za nchi kushiriki kikamilifu katika maandalizi na ufadhili wa miradi mikubwa ya miundombinu.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, tangu kujiunga na taasisi hiyo, Tanzania imeanza kunufaika kupitia maandalizi ya miradi ya kimkakati ikiwemo maendeleo ya Bandari ya Mangapwani Zanzibar, Mradi wa Mini Liquefied Natural Gas (Mini LNG), miundombinu ya usafirishaji wa umeme na upanuzi wa huduma za usafishaji wa figo (dialysis) kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).
Mkutano wa mwaka 2026 unafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “A Decade of Economic Impact: From Ambition to Delivery.”
Balozi Omar amesema katika kipindi cha siku mbili za mkutano kutakuwa na Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50, Jukwaa la Miundombinu Afrika na hafla za kusaini makubaliano mbalimbali ya maandalizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya miundombinu.
Amesema kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo, Tanzania itapata fursa ya kuendelea kujitangaza kama kitovu cha uwekezaji na maendeleo ya miundombinu Afrika Mashariki, kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za fedha za kimataifa, pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika miradi ya kimkakati yenye tija kwa maendeleo ya taifa.
“Serikali inawahakikishia wananchi kuwa maandalizi yote yanaendelea vizuri kwa ushirikiano na Africa50 pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali ili kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa mafanikio makubwa,” amesema Balozi Omar.
Ameongeza kuwa Serikali inawakaribisha wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na kuwapokea wageni watakaofika nchini kwa ajili ya mkutano huo, ambao unatarajiwa kuwa miongoni mwa mikutano mikubwa ya kimataifa itakayofanyika nchini mwaka 2026.
.jpeg)

.jpeg)
Post A Comment: