Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Mikopo kwa Dhamana za Mali Zinazohamishika wa Mwaka 2026, unaolenga kuweka mfumo bora wa usimamizi wa mikopo inayotolewa kwa kutumia mali zinazohamishika kama dhamana.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kushoto) na Naibu Mawaziri wake, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb)(Katikati) na Mhe. Laurent Luswetula (Kulia), wakisikiliza hoja za wabunge mbalimbali kuhusu Muswada wa Sheria ya Mikopo kwa Dhamana za Mali Zinazohamishika wa Mwaka 2026, uliowasilishwa, ambao unaolenga kuweka mfumo bora wa usimamizi wa mikopo inayotolewa kwa kutumia mali zinazohamishika kama dhamana.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Katikati), Naibu Mawaziri wake, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) (wanne kushoto) na Mhe. Laurent Luswetula (wa nne kulia), na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Nsubili Joshua (wa tatu kushoto), mara baada ya kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Mikopo kwa Dhamana za Mali Zinazohamishika wa Mwaka 2026, unaolenga kuweka mfumo bora wa usimamizi wa mikopo inayotolewa kwa kutumia mali zinazohamishika kama dhamana.





Na Joseph Mahumi na Peter Haule, Dodoma


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amewasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Mikopo kwa Dhamana za Mali Zinazohamishika wa Mwaka 2026, unaolenga kuweka mfumo bora wa usimamizi wa mikopo inayotolewa kwa kutumia mali zinazohamishika kama dhamana.

Akiwasilisha Muswada huo Bungeni jijini Dodoma, Mhe. Balozi Omar amesema Sheria hiyo inayopendekezwa inalenga kuongeza matumizi ya huduma za benki nchini kutoka asilimia 22 mwaka 2023 hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Mhe. Balozi Omar amesema pia Muswada huo unalenga kuongeza uwiano wa mikopo inayotolewa kwa sekta binafsi dhidi ya Pato la Taifa kutoka asilimia 22.5 mwaka 2024 hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, sambamba na kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha kufikia asilimia 20 ifikapo mwaka 2030, kutoka asilimia 17.1 mwaka 2024.

Alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kupanua wigo wa wananchi na wafanyabiashara kupata mikopo kwa kutumia mali zinazohamishika kama dhamana, badala ya kutegemea zaidi mali zisizohamishika kama vile ardhi na majengo.

Aidha Mhe. Balozi Omar alisema miongoni mwa changamoto zinazolengwa kutatuliwa na Muswada huo ni kutokuwepo kwa mfumo wa pamoja wa usajili wa mali zinazohamishika zinazoweza kutumika kama dhamana, ambapo hali hiyo imekuwa ikisababisha mali moja kutumika kama dhamana kwa mikopo mbalimbali bila wakopeshaji wengine kuwa na taarifa, jambo ambalo linaweza kuchangia kuongezeka kwa mikopo chechefu katika sekta ya fedha.

Changamoto nyingine ni kukosekana kwa usimamizi na utaratibu wa pamoja wa mali zinazohamishika zinazoweza kutumika kama dhamana, pamoja na kutokuwepo kwa utaratibu madhubuti wa utekelezaji wa haki za mkopaji na mkopeshaji wakati wa kuuza mali hizo.

Mhe. Balozi Omar, aliongeza kuwa umuhimu wa kuweka utaratibu huo unatokana pia na ukweli kwamba baadhi ya mali zinazohamishika zinaweza kupoteza thamani ndani ya muda mfupi au kuharibika.

Alibainisha kuwa Muswada huo umegawanyika katika sehemu kumi zinazoweka mfumo mpana wa kisheria wa matumizi, usajili, usimamizi na utekelezaji wa dhamana zinazotokana na mali zinazohamishika.

Mhe. Balozi Omar alisema Sehemu ya Kwanza, inahusu masharti ya utangulizi, ikiwemo jina la Sheria, kuanza kutumika kwake, matumizi ya Sheria na tafsiri ya misamiati huku Sehemu ya Pili inaanzisha masharti ndani ya Benki Kuu ya Tanzania yanayohusu dhamana na kuainisha mamlaka ya Benki pamoja na ukasimishaji wa majukumu.

Aliongeza Sehemu ya Tatu inaainisha maslahi katika dhamana kwa mkopo mmoja au zaidi, pamoja na aina za mali zinazoweza kutumika kama dhamana, zikiwemo mali zinazoshikika na zisizoshikika, zinazoweza kuhamishika au zisizoweza kuhamishika, na Sehemu hiyo pia inaweka sharti la Benki Kuu kushauriana na Waziri kabla ya kutangaza mali zinazoweza kutumika kama dhamana.

Sehemu ya Nne inahusu usajili wa maslahi katika dhamana, muda wa uhalali wa usajili, marekebisho au ufutaji wa usajili pamoja na upekuzi wa taarifa, huku Sehemu ya Tano inahusu maslahi katika dhamana dhidi ya mtu wa tatu, maslahi katika mapato yanayotokana na dhamana pamoja na utekelezaji wa maslahi katika mali zinazohamishika zilizochanganywa.

Aidha, alisema Sehemu ya Sita inaainisha vipaumbele katika maslahi ya wakopaji tofauti, mapato na malipo yanayochanganywa kwa mkusanyiko, pamoja na athari za kufilisika kwa mkopaji, ikiweka masharti kuhusu haki za wahusika mbalimbali katika matumizi ya dhamana na haki ya kipaumbele katika maslahi ya dhamana.

Kwa mujibu wa Mhe. Balozi Omar, alisema Sehemu ya Saba inaainisha haki ya kukagua dhamana, wajibu wa kutoa taarifa, jukumu la kutunza dhamana, pamoja na haki na wajibu wa mdaiwa, ambapo pia inahusu madai ya malipo yaliyofanywa na mdaiwa, haki katika makusanyo yanayotarajiwa, mali au hati za malipo zinazowezesha malipo au utekelezaji wa dhamana, pamoja na ulinzi wa haki za mkopaji.

Aliongeza kuwa Sehemu ya Nane inaweka masharti yanayohusu utekelezaji wa dhamana, ikiwemo usajili wa taarifa za utekelezaji, uondoshaji wa dhamana, matumizi ya dhamana katika kutekeleza wajibu unaotokana na mkopo na utaratibu wa uondoshaji wa dhamana.

Sehemu hiyo pia inaainisha ukomo wa maslahi katika dhamana baada ya uondoshaji, mgawanyo wa mapato, pendekezo la kumiliki dhamana katika malipo ya deni na utaratibu wa kuweka pingamizi dhidi ya pendekezo hilo. Aidha, inaweka masharti kuhusu uhifadhi wa dhamana, gharama za uhifadhi na haki ya mkopaji kuchagua sehemu mbadala ya kuhifadhi dhamana.

Mhe. Balozi Omar, alisema Sehemu ya Tisa inahusu masharti ya jumla, ikiwemo utekelezaji wa haki na wajibu, haki ya kudai fidia dhidi ya ukiukwaji wa wajibu, kinga, kosa la kutoa taarifa za uongo, malalamiko na mapitio ya maamuzi ya Benki pamoja na rufaa, ambapo Sehemu hiyo pia inampa Waziri mamlaka ya kutengeneza kanuni kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji bora wa Sheria hiyo.

Sehemu ya Kumi inaainisha marekebisho ya sheria mbalimbali pamoja na Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sheria ya Kampuni, Sheria ya Ufilisi na sheria nyingine zinazohusiana na usimamizi wa mali na masuala ya kifedha, yanayopendekezwa kufanyika ili kuwezesha utekelezaji wa Muswada huo.

Mhe. Balozi Omar, alisema kuwa kutungwa kwa Sheria hiyo kutasaidia kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa mikopo, kuimarisha usimamizi wa dhamana, kulinda haki za wakopaji na wakopeshaji, na kuchochea maendeleo ya sekta ya fedha nchini.
Share To:

Post A Comment: