Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Dkt. Mahmoud Thabit Kombo leo Julai 14, 2026 amekabidhiwa rasmi kombe kutoka kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt Ngwaru Maghembe linalotokana na ushindi wa timu ya Wanadiplomasia katika Bonanza Kuu la Bunge la Benki ya CRDB lililofanyika tarehe 20 Juni 2026 katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

Timu ya Wanadiplomasia, iliyoshirikiana na wawakilishi kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ilitwaa ubingwa baada ya kuishinda timu ya Wabunge kwa mikwaju ya penalti 5–4, kufuatia sare ya bao 1–1 katika muda wa kawaida wa mchezo.

Mechi hiyo ilikuwa kivutio kikuu cha bonanza hilo la michezo na afya, lililolenga kuimarisha afya, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa viongozi na watumishi wa taasisi mbalimbali za umma.

Aidha, ushindi wa timu hiyo ya Wanadiplomasia unaendelea kudhihirisha umuhimu wa michezo kama nyenzo ya kuimarisha mahusiano mema, urafiki na ushirikiano baina ya taasisi za Serikali na wadau wake.

Awali kombe hilo lilipokelewa na Mhe. Dkt. Ngwaru kwa niaba ya Mhe. Waziri Kombo kutoka kwa Mkuu wa Mabalozi ambaye ni Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini, Mhe. Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: