Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akizungumza na wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake wakati wa kikao kilichoandaliwa na Umoja wa Wafanyabiashara wa Mifugo na Mazao Yake Temeke (UWAMIMATE), kilichofanyika Julai 19, 2026 katika Ukumbi wa Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Temeke, Dar es Salaam. Katika kikao hicho, wafanyabiashara waliwasilisha changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya biashara ya mifugo na mazao yake, huku Waziri akiahidi kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wizara na taasisi husika
******************
-Awahimiza kuimarisha umoja wao
-Aahidi kuziwasilisha hoja kwa wizara na taasisi husika
Daudi Nyingo – DAR ES SALAAM
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema kuwa, Serikali itaendelea kusikiliza na kushughulikia changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa mifugo nchini, huku akiahidi kuziwasilisha hoja zinazohusu wizara na taasisi mbalimbali ili zipatiwe ufumbuzi.
Waziri Kakurwa alitoa kauli hiyo Julai 19, 2026, wakati wa kikao na wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake kilichofanyika katika ukumbi wa Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Temeke, Dar es Salaam. Katika kikao hicho, Umoja wa Wafanyabiashara wa Mifugo na Mazao Yake Temeke (UWAMIMATE) uliwasilisha changamoto 15 zinazoathiri biashara ya mifugo na mazao yake.
Akizungumza baada ya kupokea hoja hizo, Waziri alisema changamoto zilizowasilishwa hazihusu wafanyabiashara wa Temeke pekee, bali zinaakisi hali halisi ya wafanyabiashara wa mifugo katika maeneo mengi nchini.
“Nimepokea masuala 15 ambayo yanahitaji kujadiliwa, kuchambuliwa na kufikiwa maamuzi yatakayosaidia kupunguza changamoto, kuongeza tija katika biashara zenu na kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika uchumi wa familia na taifa,”
“Kiuhalisia, ninachokiona ni kama kikao cha uwakilishi wa wafanyabiashara wa mifugo nchini kupitia chama chenu cha UWAMIMATE,” alisema Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa.
Waziri Kakurwa aliwahimiza wafanyabiashara hao kuendelea kuimarisha umoja wao, akieleza kuwa mshikamano ni nyenzo muhimu ya kulinda maslahi yao, kushiriki katika maboresho ya sera na sheria pamoja na kuongeza nguvu ya ushawishi kwa Serikali.
Aliipongeza UWAMIMATE kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kikao hicho, akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya kujenga ajenda zinazogusa sekta nzima badala ya maslahi ya kundi moja.
“Umoja ni nguvu. Mtu mmoja mmoja hawezi kushindana katika mazingira ya leo. Kupitia umoja mnaweza kutetea maslahi yenu, kushiriki katika utungaji wa sera na kujenga sekta yenye nguvu zaidi,” aliongeza Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa..
Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Mifugo na Mazao Yake Temeke (UWAMIMATE), Bw. Joshua Lungwa, alisema umoja huo umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake kwa lengo la kujadili changamoto zinazowakabili na kutafuta suluhisho kwa kushirikiana na Serikali.
Alisema kikao hicho kimewapa wafanyabiashara fursa ya kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na kupata ufafanuzi kuhusu hatua zinazotarajiwa kuchukuliwa ili kuboresha mazingira ya biashara ya mifugo nchini.
Miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa ni ushuru wa mara ya pili kwa ng'ombe wanaotoka mikoani, utitiri wa tozo katika sekta ya mifugo na mazao yake, kuingia sokoni kwa mifugo isiyo na ubora, miundombinu duni katika minada ya mifugo, kushamiri kwa uuzaji holela wa nyama (besera), uwepo wa wafanyabiashara wa mifugo wasiotambulika kisheria (galagaja) katika minada, changamoto za vibali vya uuzaji wa mifugo minadani,
Changamoto nyingine ni faini zinazotozwa wainuaji wa mifugo kwenye magari ya kubebea ng'ombe, changamoto ya soko la ngozi, hitaji la ujenzi wa machinjio katika Wilaya ya Temeke, upatikanaji wa fursa za soko la nyama nje ya nchi, matumizi ya Power of Attorney kwa wainuaji wa mifugo kwenye magari ya kubebea mifugo, madai ya leseni ya uchinjaji katika eneo la Kibaha pamoja na changamoto za uongozi katika baadhi ya minada ya mifugo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akizungumza na wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake wakati wa kikao kilichoandaliwa na Umoja wa Wafanyabiashara wa Mifugo na Mazao Yake Temeke (UWAMIMATE), kilichofanyika Julai 19, 2026 katika Ukumbi wa Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Temeke, Dar es Salaam. Katika kikao hicho, wafanyabiashara waliwasilisha changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya biashara ya mifugo na mazao yake, huku Waziri akiahidi kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wizara na taasisi husika
Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akiwa na viongozi na wanachama wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Mifugo na Mazao Yake Temeke (UWAMIMATE), pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo, mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kujadili changamoto na fursa za biashara ya mifugo na mazao yake, kilichofanyika Julai 19, 2026 katika Ukumbi wa Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Temeke, Dar es Salaam.








Post A Comment: