Serikali ya Tanzania na Marekani zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Afya (MoU) ya miaka mitano yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.14, hatua inayotarajiwa kuimarisha mfumo wa huduma za afya nchini huku ikijenga msingi wa kujitegemea katika utoaji wa huduma hizo.
Makubaliano hayo yatatekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2030 kupitia uwekezaji wa pamoja wa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Marekani.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dar es Salaam Julai 1, 2026, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa amesema Serikali ya Marekani imekusudia kuwekeza takribani dola bilioni 1.34, huku Serikali ya Tanzania ikiahidi kuchangia zaidi ya dola bilioni 1.8 katika kipindi hicho.
Amesema ushirikiano huo mpya unaashiria mwelekeo mpya wa mahusiano kati ya mataifa hayo mawili, ukijengwa katika misingi ya usawa, uwajibikaji na kuongeza uwezo wa Tanzania kugharamia mfumo wake wa afya kwa kutumia rasilimali za ndani.
“Makubaliano haya si mwendelezo wa utegemezi bali ni ramani ya kutuondoa kwenye utegemezi. Ifikapo mwaka 2030 Tanzania ndiyo itakayobeba sehemu kubwa ya gharama za mfumo wake wa afya,” alisema Mchengerwa.
Alieleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha huduma muhimu za afya zinaendelea kutolewa kwa ufanisi kwa kugharamia mishahara ya watumishi wa afya, ununuzi wa dawa, vifaa tiba, huduma za maabara pamoja na maeneo mengine muhimu kupitia mapato ya ndani.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa falsafa ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ya kujitegemea na kujenga taifa lenye uwezo wa kugharamia maendeleo yake.
Mchengerwa pia aliishukuru Serikali na wananchi wa Marekani kwa mchango mkubwa walioutoa kwa Tanzania kupitia programu mbalimbali za afya, hususan Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR), ambao kwa zaidi ya miongo miwili umechangia kuimarisha huduma za kinga, tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI pamoja na kuimarisha mifumo ya afya nchini.
Alisema ushirikiano huo mpya unalenga kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana kupitia programu za awali yanadumishwa huku Tanzania ikiendelea kuongeza uwezo wa kujitegemea katika kugharamia na kusimamia sekta yake ya afya kwa ufanisi.















Post A Comment: