Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S.Johari amesema kuwa, Sheria zinapaswa kutumika kama nyenzo ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kufungua fursa, kuongeza uwajibikaji, kuvutia uwekezaji, kuongeza mapato ya Serikali, kuboresha elimu na afya.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo, wakati wa Uzinduzi wa Kitabu kipya kiitwacho " Falsafa ya Sheria ya Mama Samia: Utekelezaji wake katika Mageuzi ya Kiuchumi na Kijamii, ulioratibiwa na Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzani n kufanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Julai 10, 2026.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesisitiza kuwa,thamani ya Sheria hupimwa kwa uwezo wake wa kuboresha maisha ya wananchi, kuvutia uwekezaji,kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa Wananchi.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa, wazo la kuandika kitabu hicho lilitokana na tafakuri ya kina kuhusu nafasi ya sheria katika kuchochea maendeleo, ambapo waandishi wa Kitabu hicho walitaka kujibu maswali muhimu kuhusu namna marekebisho ya sheria, mabadiliko ya sera na maboresho ya taasisi yalivyochangia kuleta matokeo chanya katika uchumi na ustawi wa jamii.
"Kitabu hiki hakikuandikwa kwa lengo la kusifu tu mazuri yaliyofanyika, , bali ni hii kazi ya uchambuzi wa kitaaluma inayotumia ushahidi, takwimu na nyaraka rasmi kuchunguza kama mageuzi ya kisheria na kisera yaliyofanyika tangu Machi mwaka 2021 yanaonesha mfumo unaoweza kueleweka, kupimwa na kujadiliwa kitaaluma. Amesema Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mhe. Johari amefafanua kuwa, lengo kuu lilikuwa kuhamisha mjadala kutoka kwenye kauli za jumla kwenda kwenye ushahidi wa kisayansi kwa kuangalia matokeo halisi ya marekebisho ya sheria na sera kwa wananchi.







Post A Comment: