Serikali imezitaka Wizara, Taasisi za Umma, Sekta Binafsi, Watafiti na Mashirika ya Kiraia kuchangamkia fursa ya Tanzania kuwa mwenyeji wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP 12).
Hayo yamesemwa leo Julai 2, 2026 Jijini Tanga na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu maandalizi ya Tanzania kuelekea Mkutano huo unaotarajia kufanyika nchini kuanzia tarehe 6-9 Oktoba mwaka huu.
Naibu Waziri Kwagilwa amesema katika Mkutano wa 11 wa Nchi Wanachama uliofanyika nchini Madagasca mwaka 2024, Tanzania ilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Mkataba wa Nairobi kwa kipindi cha miaka miwili hadi Disemba Mwaka 2026 pamoja na kuteuliwa kuwa mwenyeji wa COP12.
“Mkutano wa COP12 utajadili utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mkataba kwa kipindi cha mwaka 2024–2026 pamoja na kujadili masuala muhimu ikiwemo hifadhi na urejeshwaji wa mifumo ikolojia ya bahari kama mikoko, miamba ya matumbawe na nyasi bahari” amesema Mhe. Kwagilwa.
Ameongeza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuipa kipaumbele sekta ya mazingira na uhifadhi wa rasilimali za bahari ili kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za bahari, mito, maziwa, maji chini ya ardhi na maeneo oevu.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Kwagilwa, amesema Dira 2050 imeitambua sekta ya uchumi wa Buluu kuwa miongoni mwa sekta za kimkakati zinazokusudia kuleta mageuzi ya maendeleo endelevu na kuchangia ukuaji wa kijamii, kiuchumi na kiikolojia.
Amesema kuwa Tanzania ni nchi ya pwani yenye fursa kubwa ya kunufaika na sekta ya uchumi wa buluu kupitia uvuvi, nishati, usafirishaji, utalii, madini, mazingira na viwanda, hivyo mkutano huo utaliwezesha taifa kuwa katika nafasi bora ya kufikia maendeleo endelevu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian amesema matokeo ya utafiti uliofanyika mkoani humo yanaonyesha athari za mabadiliko ya tabianchi zimeanza kuathiri kwa kiwango kikubwa shughuli za uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji, hususan kilimo cha mwani.
Amesema utafiti uliofanyika kati ya mwaka 2021 na 2025 umebaini kuwa joto la bahari limeongezeka kutoka nyuzi joto 25.6 mwaka 2021 hadi kufikia nyuzi joto 28.39 mwaka 2024, hali inayobadili mfumo wa ikolojia wa bahari na kuathiri uzalishaji katika sekta ya uvuvi.
"Tumeshuhudia ongezeko la karibu nyuzi joto tatu baharini, huku siku za wavuvi kwenda kuvua zikishuka kutoka siku 221 mwaka 2021 hadi siku 170 kutokana na upepo mkali na hatari ya usalama baharini. Pia mavuno ya samaki yamepungua kwa wastani wa asilimia 25 hadi 30," amesema Dkt. Burian.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda amesema mkutano wa COP 12 utahusisha washiriki takribani 500-600 ikiwemo viongozi wa nchi, wataalamu na wadau mbalimbali.
Ameongeza kuwa lengo la tamko hilo la Serikali ni kuweka msingi wa maandalizi ya kina, ikiwa ni pamoja na kubainisha vipaumbele vya Taifa, na kupanga mikakati ya ushiriki ili kuhakikisha maandalizi yanafanyika kwa ufanisi na kwa wakati.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Nairobi unaohusu Hifadhi, Usimamizi na Uendelezaji wa Mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Mkataba huu ulisainiwa tarehe 21 Juni 1985 na unatekelezwa chini ya usimamizi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).
MWISHO









Post A Comment: