• Akagua miradi ya maendeleo, ahimiza ikamilike kwa wakati.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu, amewaletea wananchi wa Mlimba kiasi cha Shilingi Bilioni 1.2 za kitanzania kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili za msingi zitakazoongeza fursa za elimu na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Prof. Shemdoe amesema hayo Julai 3, 2026 katika Uwanja wa Tandare, Kata ya Igima, wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi hao, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhimiza uwajibikaji wa watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba.
"Leo nimekuja na habari njema kutoka kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaletea Shilingi
Bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa Shule za Msingi Mgeta na Nganyangira. Nimejiridhisha kuwa fedha hizo tayari zimeingizwa kwenye akaunti ya halmashauri ili utekelezaji uanze mara moja," ameeleza Prof. Shemdoe.
Katika ziara hiyo, Prof. Shemdoe amezindua mabasi mawili ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, amefungua Shule ya Msingi Ngajengwa na kukabidhi vipaza sauti kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii ili kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi katika maeneo yao.
Aidha, Prof. Shemdoe amekagua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba saba za watumishi, kukagua ujenzi wa wodi mbili za upasuaji katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, pamoja na kutembelea barabara inayojengwa ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikisababisha usumbufu kwa wananchi.
"Nimetembelea daraja kubwa linalojengwa katika Kata ya Mgeta ambalo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Shilingi Bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wake. Vilevile, kuna daraja lingine limepatiwa
Shilingi Bilioni 1.7. Huu ni uwekezaji mkubwa unaoonyesha dhamira ya Mhe. Rais ya kuwaletea wananchi maendeleo," amesema Prof. Shemdoe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima amesema Wilaya ya Mlimba ndiyo kinara wa uzalishaji katika mkoa huo, huku akibainisha kuwa mapato ya halmashauri hiyo yanaendelea kuongezeka kwa kasi kuliko halmashauri nyingine kutokana na kuimarika kwa shughuli za uzalishaji na ukusanyaji wa mapato.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Mhe. Dkt. Kellenrose Rwakatare amesema Serikali inaendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga na kuimarisha miundombinu ya shule, ikiwemo kukamilisha majengo yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi, hatua inayochangia kuwapatia wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia.











Post A Comment: