Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, amewahimiza Watanzania wanaotembelea Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutembelea Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi zake ili kupata elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali.

Prof. Kabudi ametoa wito huo leo, Julai 4, 2026, baada ya kutembelea banda hilo na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi zake. Amesema banda hilo limeandaliwa kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu na huduma zinazotolewa, sambamba na kupokea maoni, kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Amesisitiza kuwa maafisa waliopo katika banda hilo hawatoi elimu pekee, bali pia wanatoa ushauri wa kitaalamu na kuwaelekeza wananchi namna ya kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili kupitia taasisi husika.

“Nawahamasisha wananchi wenye changamoto mbalimbali au wanaohitaji kupata ufumbuzi wa masuala yanayowakabili watembelee Banda la Ofisi ya Waziri Mkuu. Hapa watapata ushauri, maelekezo na huduma zitakazowasaidia kutatua changamoto zao,” amesema Prof. Kabudi.

Aidha, amesema Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2026 yanafanyika katika kipindi ambacho nchi imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo yamekuwa jukwaa muhimu la kuonesha mafanikio ya Serikali na kuelimisha wananchi kuhusu mchango wa taasisi mbalimbali katika kufanikisha dira hiyo.

Prof. Kabudi ameeleza kuwa kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania inalenga kujenga Taifa jumuishi, lenye ustawi, haki, amani na linalojitegemea kiuchumi, huku akisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika kupata elimu na kutumia huduma zinazotolewa na taasisi za Serikali ni nguzo muhimu katika kufikia malengo hayo.
Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: