Na. Peter Haule, WF, Arusha

 

Serikali imesema matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) yameendelea kuongezeka nchini, hatua iliyochangia kuimarika kwa uwazi, ushindani, uwajibikaji na matumizi yenye tija ya fedha za umma katika shughuli za ununuzi na ugavi.

 

Hayo yalielezwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila, wakati wa Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma 2026 lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

 

Alisema kuwa hadi Juni 30, 2026, jumla ya wazabuni 45,270 walikuwa wameidhinishwa na kusajiliwa katika Mfumo huo, ambapo asilimia 95 kati yao walikuwa wazabuni wa ndani.

 

“Katika mwaka wa fedha 2025/2026, hadi Juni 30, 2026, jumla ya tuzo za zabuni 181,057 zenye thamani ya shilingi trilioni 14.5 zilitolewa kupitia mfumo wa NeST, hatua inayoonesha kuongezeka kwa matumizi ya Mfumo huo katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma”, alisema Dkt. Nguvila.

 

Dkt. Nguvila alisema mafanikio hayo yanaonesha kuwa NeST imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha usimamizi wa shughuli za ununuzi wa umma na ugavi, pamoja na kuongeza uwazi, ushindani na thamani ya fedha za umma.

 

Alisema Mfumo huo pia umeipa Tanzania heshima kimataifa baada ya kuchaguliwa kuwa miongoni mwa Mifumo 20 bora ya Serikali duniani katika Tuzo za World Summit on the Information Society, mafanikio yanayoakisi hatua kubwa iliyopigwa katika mageuzi ya kidijitali kwenye sekta ya ununuzi wa umma na ununuzi endelevu.

 

Dkt. Nguvila alifafanua kuwa, ujenzi wa Mfumo wa NeST umekamilika kwa asilimia 100 na kwa sasa shughuli zote muhimu za ununuzi wa umma, kuanzia usajili wa wazabuni, uandaaji wa zabuni, usimamizi wa mikataba hadi malipo, zinafanyika kupitia Mfumo huo.

 

Alisisitiza kuwa taasisi zote za umma zina wajibu wa kutekeleza shughuli za ununuzi kupitia Mfumo wa NeST, akionya kuwa taasisi yoyote itakayofanya ununuzi nje ya Mfumo huo itakuwa imekiuka matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma.

 

"Serikali itaendelea kusimamia matumizi ya Mfumo wa NeST ili kuhakikisha taasisi zote za umma zinafuata sheria na taratibu zilizowekwa," alisema Dkt. Nguvila.

 

Aidha, Dkt. Nguvila aliipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma na kuimarisha matumizi ya Mfumo wa NeST, ambapo aliitaka Mamlaka hiyo kuendelea kuuboresha Mfumo huo na kuuunganisha na mifumo mingine ya Serikali ili kuongeza ufanisi, kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa na kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.

 

Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kutambua ununuzi wa umma kama nyenzo muhimu ya sera ya uchumi inayochochea maendeleo ya viwanda vya ndani, kukuza ushiriki wa wazabuni wazawa, kuongeza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa pamoja na kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba, alisema taasisi zote za Serikali zinapaswa kuzingatia kikamilifu Sheria ya Ununuzi wa Umma, akisisitiza kuwa taasisi zitakazoshindwa kutekeleza matakwa ya sheria hiyo zitawekwa hadharani, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Bw. Simba pia aliwapongeza wadau walioshiriki Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma 2026 na kuwataka kutumia fursa hiyo kuongeza uelewa na uwezo wa kitaalamu ili kuendelea kuboresha utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma nchini.

Share To:

Post A Comment: