Maofisa Utumishi nchini wameagizwa kushirikiana kwa karibu na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuhakikisha taarifa za watumishi wanaokaribia kustaafu zinajazwa na kuwasilishwa kwa usahihi na kwa wakati, ili kuondoa malalamiko yanayotokana na ucheleweshaji wa mafao.

Agizo hilo limetolewa jijini Arusha na Katibu Tawala Wilaya ya Arusha, Dk. Jacob Rombo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dk,Toba Nguvila, wakati akifungua mafunzo kwa waajiri na maofisa wanaoshughulikia masuala ya wanachama wa PSSSF kutoka taasisi mbalimbali za umma mkoani Arusha.

Dk, Nguvila alisema changamoto nyingi za ucheleweshaji wa mafao na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wastaafu husababishwa na taarifa kutokamilika au kutowasilishwa kwa wakati na waajiri.

Alisema maofisa utumishi wanapaswa kuhakikisha taarifa za watumishi wanaokaribia kustaafu zinahakikiwa na kuwasilishwa mapema ili kuwawezesha kupata mafao yao bila usumbufu. 

"Kila mtumishi anakuwa na kumbukumbu rasmi za utumishi wake kuanzia anapoajiriwa hadi anapostaafu. Ni muhimu nyaraka zote zihifadhiwe vizuri na zipatikane kwa urahisi pale zinapohitajika ili walipwe mafao yao kwa mkupuo," alisema.

Aliongeza kuwa maofisa utumishi wanapaswa kuwahudumia watumishi na wananchi kwa weledi, kutoa taarifa sahihi na kushughulikia changamoto zao kwa wakati ili kuondoa usumbufu usio wa lazima.

Kwa upande wake, Meneja wa PSSSF Kanda ya Kaskazini Magharibi, Yessaya Mwakifulefule, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo  maofisa hao kuhusu maboresho na huduma mpya zinazotolewa na mfuko, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika kuharakisha uchakataji wa mafao.

Alisema mafanikio ya utaratibu wa kulipa mafao kwa wakati yanategemea ushirikiano wa waajiri, hususan maafisa rasilimali watu, kwa kuhakikisha taarifa za watumishi zinawasilishwa na kukamilishwa mapema.

"Mfuko wetu unaendelea na mpango wa kuhakikisha wastaafu wanalipwa mafao yao siku moja kabla ya kustaafu sisi PSSSF tunasema  'tunalipa jana' "

Alifafanua kuwa taarifa zote za michango zinapokamilishwa kwa wakati, mfuko huweza kukokotoa na kulipa mafao kwa asilimia 100 kabla ya mtumishi kustaafu rasmi na kutoa rai kwa maofisa rasilimali watu kuendelea kufuatilia na kuhakiki taarifa za watumishi wanaokaribia kustaafu ili kuhakikisha wanapata mafao yao kwa wakati na bila changamoto.













Share To:

Post A Comment: