Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema serikali imechukua hatua madhubuti kumaliza changamoto za kukatika kwa umeme zilizokuwa zikiathiri baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, hali iliyokuwa ikisababisha wilaya nzima kukosa umeme pindi hitilafu zinapotokea kwenye baadhi ya sehemu za mtandao.
Ndejembi amebainisha hayo leo wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Usambazaji Umeme (Switching Station) pamoja na transfoma mpya zilizojengwa kwa lengo la kuimarisha na kudhibiti mfumo wa usambazaji umeme katika wilaya hiyo.
Amesema uwepo wa miundombinu hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya mgao wa umeme wa ghafla, ambao hapo awali ulikuwa ukisababisha maeneo mengi ya Kongwa na wilaya jirani kuathirika pindi hitilafu inapotokea sehemu moja ya mfumo.
“Kwa muda mrefu, changamoto ya voltage ndogo na kukatika kwa umeme mara kwa mara ilikuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi na wajasiriamali wadogo, hususan waliokuwa wakishindwa kuendesha shughuli za uzalishaji kama kusaga nafaka na kukamua mafuta kutokana na uhaba wa umeme wa uhakika,” amesema Ndejembi.
Ameongeza kuwa serikali, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuliweka sekta ya nishati katika kipaumbele cha juu, hali iliyowezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Amesema zaidi ya shilingi bilioni 10 zimewekezwa katika eneo la Mbande kwa ajili ya ujenzi wa Switching Station hiyo, hatua ambayo itanufaisha wakazi wa wilaya za Kongwa, Kiteto, Gairo, Chamwino na Mpwapwa kwa kupata umeme wa uhakika na wa kutosha.
“Lengo letu siyo tu kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa kuwasha taa, bali ni umeme wa kuendesha viwanda na shughuli za uzalishaji. Hii itasaidia kukuza uchumi wa maeneo haya na kuongeza fursa za ajira,” ameongeza.
Uzinduzi wa mradi huo unatajwa kuwa sehemu ya jitihada za serikali kuboresha miundombinu ya nishati nchini na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika unafika kwa wananchi wengi zaidi, hususan maeneo ya vijijini na pembezoni.



.jpeg)


.jpeg)
Post A Comment: