SERIKALI imezindua jukwaa jipya la kitaifa la ubunifu litakalowawezesha wanasayansi, watafiti na wabunifu kubuni suluhisho za ndani kwa changamoto zinazoikabili nchi katika sekta za afya, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabianchi na teknolojia, hatua inayotarajiwa kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Jukwaa hilo linalofahamika kama Grand Challenges Tanzania (GC-TZ) linalenga kuunganisha watafiti, watunga sera, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu katika kutatua changamoto za maendeleo na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Akizindua jukwaa hilo jijini Dodoma tarehe 04 Juni, 2026, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidhi Ameir, alisema mpango huo umeanzishwa wakati Tanzania inaanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi shindani, unaojitegemea na unaowajumuisha wananchi wote.
Alisema pamoja na mafanikio yaliyopo, nchi inaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, kisukari, magonjwa ya figo na moyo, ambayo yanahitaji suluhisho bunifu na endelevu.
Alisema kufanikisha malengo ya Dira ya 2050 kunahitaji uwekezaji mkubwa na endelevu katika tafiti na ubunifu unaolenga kujibu changamoto halisi zinazowakabili wananchi.
“Mpango huu utachochea maendeleo ya teknolojia nafuu za uchunguzi wa magonjwa, utengenezaji wa dawa, chanjo, vifaa tiba na mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa. Pia utasaidia kuongeza uzalishaji wa kilimo, kuimarisha usalama wa chakula, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuhifadhi rasilimali za asili na kupanua matumizi ya nishati safi,” alisema.
Alisema mafanikio ya jukwaa hilo yatategemea ushirikiano wa karibu kati ya watafiti, taasisi za Serikali, Sekta binafsi, taasisi za fedha, washirika wa maendeleo na wananchi kwa ujumla.
Aidha, alisema Serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa kitaifa wa tafiti na ubunifu kupitia uwekezaji katika tafiti za kisayansi na programu mbalimbali za ubunifu zinazosimamiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na taasisi nyingine.
Aliwataka wadau kutoka sekta za umma na binafsi, taasisi za utafiti, mashirika ya kiraia na washirika wa maendeleo kuunga mkono jukwaa hilo ili kuhakikisha linatoa matokeo yanayotarajiwa kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, alisema uzoefu wa kimataifa unaonyesha kuwa ubunifu unaoongozwa na changamoto maalumu huleta matokeo makubwa pale ambapo vipaji, rasilimali, ushirikiano na malengo uunganishwa.
Alisema Tanzania tayari imeweka msingi imara wa maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu, ambapo zaidi ya Sh bilioni 129 zimekusanywa kupitia Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya kusaidia tafiti, ubunifu, maendeleo ya teknolojia na ujenzi wa miundombinu ya kisayansi.
Alisema kati ya fedha hizo, Serikali imechangia zaidi ya Sh bilioni 85, jambo linalodhihirisha dhamira yake ya kuendeleza tafiti na ubunifu nchini.
“Tanzania ina watafiti na wabunifu wenye uwezo mkubwa. Hatua inayofuata ni kuimarisha zaidi uhusiano kati ya tafiti zinazofanyika na matokeo ya maendeleo yanayohitajika na wananchi,” alisema.
Alisema katika hatua za mwanzo, GC-TZ itajikita katika maeneo manne ya kipaumbele ambayo ni afya, usalama wa chakula na lishe, mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa mazingira, pamoja na mageuzi ya kidijitali na teknolojia zinazoibukia.
Vilevile kwa upande wake Profesa Ladislaus Mnyone alibainisha kuwa ili Tanzania ifikie malengo makubwa ya Dira ya 2050 ikiwemo kuwa na uchumi wa dola trilioni moja na kuongeza pato la wastani la kila mwananchi ni lazima iwekeze kwa dhati katika rasilimali watu, kuongeza uzalishaji, na kukuza thamani ya bidhaa zetu (value addition).
Alieleza kuwa nchi inapoteza kati ya dola milioni 300 hadi 400 kila mwaka kwa kusafirisha malighafi ghafi, jambo linalofanya mabadiliko kuelekea teknolojia ya ndani kuwa hitaji la lazima na sio la hiari tena.
Ili kufanikisha maono haya, alisisitiza kuwa Serikali imeshajenga misingi imara kwa kukamilisha Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Sayansi na Teknolojia (National STI Master Plan) na kuweka madawati ya utafiti katika halmashauri 90 nchini.
Profesa Mnyone alihitimisha kwa kuonyesha kuwa chombo kipya cha Grand Challenges Tanzania kitakuwa nguzo kuu ya kuibua na kufikisha teknolojia hizi za ndani kwenye jamii, huku kikichochea sekta za afya, kilimo, na uchumi ili kuliweka taifa mstari wa mbele kiteknolojia barani Afrika.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Afya ya Ifakara (Ifakara Health Institute), Honorati Masanja, alisema ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kuendesha shughuli za utafiti na ubunifu ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa suluhisho za maendeleo.
Uzinduzi wa Grand Challenges Tanzania pia uliambatana na kutangazwa rasmi kwa mwito wa kuwasilisha mapendekezo ya tafiti zinazolenga kuboresha afya na lishe ya mama, mtoto mchanga na mtoto, ikiwa ni fursa ya kwanza ya ufadhili chini ya jukwaa hilo jipya la kitaifa la ubunifu.















Post A Comment: