Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Felchesmi Mramba, amefanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa sekta ya nishati kuhusu fursa za kuendeleza miradi ya jotoardhi na kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania.

Mazungumzo hayo yamefanyika pembeni mwa Mkutano wa Dunia wa Jotoardhi (World Geothermal Congress – WGC 2026)  nchini Canada, ambapo Mha. Mramba alikutana na Bw. Yvan Champagne, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Hewa Ukaa wa Kampuni ya CarbonAI. 

Katika kikao hicho viongozi hao wamejadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia pamoja na upatikanaji wa fedha kupitia mfumo wa hewa ukaa (carbon financing) kwa ajili ya kufadhili miradi hiyo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mha. Mramba ameikaribisha CarbonAI kushirikiana na Serikali katika kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

 Amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na taasisi na kampuni zenye teknolojia na uzoefu utakaosaidia kufikiwa kwa malengo ya maendeleo endelevu katika sekta ya nishati.

Aidha, Mha. Mramba amefanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa nishati jadidifu, hususan katika eneo la jotoardhi, kuhusu fursa za kuharakisha maendeleo ya miradi ya rasilimali hiyo nchini.

 Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuweka msisitizo mkubwa katika matumizi ya nishati jadidifu kama sehemu ya mkakati wa kuhakikisha asilimia 75 ya umeme nchini inazalishwa kutoka katika vyanzo vya nishati jadidifu ifikapo mwaka 2030.

Mkutano wa Dunia wa Jotoardhi (WGC 2026) umewakutanisha viongozi wa Serikali, Wataalam, wawekezaji na wadau wa Sekta ya Nishati kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kujadili maendeleo ya teknolojia, sera na uwekezaji katika miradi ya jotoardhi.






Share To:

Post A Comment: