Na Mwandishi Wetu

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imesema matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika sekta ya mifugo yataimarisha masoko na kuongeza ushindani wa bei ya bidhaa hiyo nchini.

Akizungumza Juni 19, 2026 katika Maonesho ya Mifugo na Mnada wa Kimataifa yanayofanyika katika Shamba la Mbogo, Chalinze mkoani Pwani, Afisa Ubora wa WRRB, Anatolius Kabyemera, amesema bodi hiyo imeingia kwenye sekta hiyo kwa lengo la kuwawezesha wafugaji kuuza mifugo yao kupitia mfumo rasmi na wenye tija.

Amesema mfumo huo utasaidia wafugaji kuimarisha ufugaji na kuongeza kipato chao ambapo mifugo itahifadhiwa kwenye eneo maalumu lililosajiliwa kama ghala ya mifugo wakati wakisubiri mnada.

“Mfumo huu utawezesha mifugo kuletwa kwenye ghala ambalo ni eneo teule lenye maji, malisho na wataalamu wa mifugo, litahesabika kuwa ghala la mifugo. Baada ya mfugaji kuingiza mifugo yake katika ghala akisubiri mnada, atapatiwa stakabadhi itakayomwezesha kupata mkopo kupitia taasisi za fedha ambazo tumeshaingia nazo makubaliano, kwa mfano NBC,” amesema Kabyemera.

Kwa upande wake, mmoja wa wafugaji waliotembelea banda la WRRB katika maonesho hayo, Moringe Gasper, ameipongeza bodi hiyo kwa kutoa elimu kuhusu matumizi ya mfumo huo katika sekta ya mifugo.

Amesema wafugaji wengi wako tayari kuona utekelezaji wa mfumo huo unaanza haraka ili nao waweze kunufaika kama ilivyo kwa wakulima wanaotumia mfumo wa stakabadhi za ghala kwa sasa.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: