Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt Maulid J. Maulid leo umefungua Mafunzo ya Uongozi wa Kimkakati (Strategic Leadership) kwa viongozi wa shule za sekondari wa Manispaa ya Shinyanga, yakiwakutanisha washiriki 44 wakiwemo Wakuu wa Shule za Sekondari 22 na Makamu Wakuu wa Shule 22. 

Mafunzo haya yanatolewa na ADEM kwa kushirikiana na African Centre for School Leadership (ACSL) kupitia VVOB kwa kufadhiliwa na Mastercard Foundation.

Akifungua mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid, alisisitiza umuhimu wa uongozi wa kimkakati katika kuimarisha utendaji wa taasisi za umma na kufanikisha malengo ya maendeleo ya sekta ya elimu.

“Uongozi wa kimkakati ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha taasisi za umma zinafikia malengo yake kwa ufanisi. Viongozi wanapaswa kuwa na uwezo wa kutazama mbele, kupanga kwa weledi na kusimamia rasilimali zilizopo ili kuleta matokeo chanya kwa taasisi wanazoziongoza,” alisema Dkt. Maulid.

Aidha, Dkt. Maulid alieleza kuwa mafunzo hayo yanatekelezwa kwa kutumia mfumo wa kisasa wa ufundishaji unaowapa washiriki fursa ya kujifunza kwa vitendo, kubadilishana uzoefu na kupata maarifa yatakayowawezesha kukabiliana na changamoto za kiuongozi katika mazingira yao ya kazi.

“Mafunzo haya yanaendeshwa kwa mfumo wa kisasa utakaohakikisha kunakuwa na mawasiliano ya mara kwa mara, lengo kuu likiwa ni kutoa nafasi kwa washiriki kutoa mrejesho kwa wazeshaji kuhusiana na maendeleo ya utekelezaji wa mada. Tunatarajia washiriki wote watatumia kikamilifu fursa hii kujifunza na kujijengea uwezo zaidi,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu huyo alibainisha kuwa washiriki watakaofanya vizuri katika mafunzo hayo watatambuliwa na kutunukiwa vyeti, hatua inayolenga kuongeza motisha na kuhamasisha ushiriki wenye tija katika mchakato mzima wa kujifunza.

Sambamba na hilo, Dkt. Maulid alisisitiza umuhimu wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa maarifa na ujuzi unaotolewa katika mafunzo hayo, akieleza kuwa mafanikio ya programu hiyo yatapimwa kupitia mabadiliko chanya yatakayoonekana katika usimamizi na utendaji wa shule husika.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: