NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imezindua filamu ya “Kifurushi” itakayooneshwa katika mabasi yanayosafiri mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mbinu zinazotumiwa kusafirisha dawa za kulevya na madhara yatokanayo na vitendo hivyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa filamu hiyo leo Juni 12, 2026 katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema hatua hiyo ni sehemu ya kampeni ya elimu kwa umma inayolenga kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia vyombo vya usafiri wa umma.
Kamishina Lyimo amesema dawa za kulevya zinaendelea kuwa tishio kwa afya za wananchi, ustawi wa familia, usalama wa jamii na maendeleo ya taifa kutokana na kuchochea changamoto za kiafya, uhalifu, kuvuruga amani na kudhoofisha nguvu kazi ya taifa, hususan kwa vijana.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya kupitia operesheni za ukamataji, uchunguzi wa makosa ya dawa za kulevya, utoaji wa tiba kwa waathirika pamoja na kampeni za elimu kwa umma.
Kwa mujibu wa Lyimo, mamlaka hiyo imebaini ongezeko la matumizi ya mbinu mbalimbali za kusafirisha dawa za kulevya, ikiwemo kuzificha kwenye mizigo na vifurushi vinavyosafirishwa kwa kutumia mabasi na vyombo vingine vya usafiri wa umma.
Amesema baadhi ya wananchi, abiria na hata wahudumu wa vyombo vya usafiri wamejikuta wakikabiliwa na mashtaka ya dawa za kulevya baada ya kubeba mizigo au vifurushi wasivyovifahamu.
“Filamu hii imeandaliwa kuonesha uhalisia wa namna mtu anavyoweza kuingia kwenye mtego wa kusafirisha dawa za kulevya kwa kubeba mzigo au kifurushi asichokifahamu pamoja na madhara ya kijamii na kiuchumi yanayoweza kujitokeza,” amesema Kamishna Lyimo.
Ameeleza kuwa DCEA ilifanya majadiliano na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja na Bodi ya Filamu Tanzania na kukubaliana kuandaa filamu hiyo ili iwe sehemu ya elimu endelevu kwa wasafiri na wadau wa sekta ya usafiri nchini.
Amesema kaulimbiu ya kampeni hiyo ni “Usafiri Salama Bila Dawa za Kulevya”, ikilenga kuhamasisha wananchi kuwa makini na mizigo au vifurushi wanavyopewa kubeba au kusafirisha kwa niaba ya watu wengine.
Aidha, amewataka wamiliki wa mabasi, makampuni ya usafirishaji na wadau wengine wa sekta hiyo kuhakikisha filamu hiyo inaoneshwa katika vyombo vyao vya usafiri ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuifanya kila safari kuwa fursa ya utoaji wa elimu.
Lyimo amesema Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kilichaguliwa kwa uzinduzi huo kutokana na kuwa moja ya vituo vikubwa vinavyohudumia maelfu ya wasafiri kila siku, hivyo kutoa nafasi ya ujumbe huo kuwafikia wadau wengi kwa wakati mmoja.
Amehimiza wananchi kutokubali kubeba mizigo, vifurushi au bidhaa wasizozifahamu, akisisitiza kuwa kifurushi kinachoonekana cha kawaida kinaweza kuwa na dawa za kulevya na kusababisha madhara makubwa ya kisheria na kijamii kwa mhusika.
“Usikubali kubeba mzigo, kifurushi au bidhaa yoyote usiyoifahamu. Hakikisha unatambua unachobeba, kinatoka kwa nani na kinaelekea kwa nani,” alisisitiza.

















Post A Comment: