Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Franklin Rwezimula, amewataka watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuendelea kuzingatia weledi, maadili na mshikamano katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi wa huduma za kisheria na kulinda maslahi ya taifa.
Rwezimula aliyasema hayo wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wa mwaka 2025/2026 uliofanyika katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha, ambapo aliwataka watumishi kutumia mkutano huo kujijengea maarifa, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kazini.
Alisema kupitia mkutano huo, washiriki watapata mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku pamoja na kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ushindani wa kiuchumi na mahitaji ya sasa ya utumishi wa umma.
“Mbali na mafunzo na mada mtakazopata katika mkutano huu, ninaamini pia mtapata fursa ya kujadili masuala muhimu yanayohusu ustawi wa ofisi yetu, kujenga mshikamano, utu na umoja miongoni mwetu kama familia moja,” alisema Rwezimula.
Aidha, aliwataka watumishi kuendelea kujiendeleza kitaaluma kwa kutumia fursa mbalimbali za mafunzo zinazotolewa ndani na nje ya nchi, akisisitiza kuwa elimu na utaalamu ni msingi muhimu wa kulinda rasilimali za taifa.
Katika hotuba yake, Rwezimula alisema Serikali ipo tayari kushirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kuimarisha uwezo wa watumishi pamoja na kuandaa wataalamu watakaokidhi mahitaji ya taifa katika sekta ya sheria na usimamizi wa mikataba.
Kwa upande wake,Wakili Mkuu wa Serikali Dk Ally Possi alisema Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inaendelea kutekeleza jukumu lake la kulinda maslahi ya taifa kupitia usimamizi wa mashauri ya serikali, ushauri wa kisheria na usimamizi wa mikataba mikubwa ya maendeleo.
Alisema mawakili wa serikali ni “askari wa kalamu” wenye jukumu kubwa la kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha fedha za umma zinalindwa kupitia usimamizi madhubuti wa mikataba na mashauri ya serikali.
“Ni muhimu taasisi zote za serikali kuwashirikisha mawakili wa serikali kuanzia hatua za maandalizi ya mikataba, majadiliano hadi utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo,” alisema Dk Possi.
Alibainisha kuwa kupitia usimamizi wa mashauri mbalimbali, ofisi hiyo imefanikiwa kuokoa fedha za serikali zinazokadiriwa kufikia trilioni 1.35, hatua aliyosema inaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha ofisi hiyo na watumishi wake.
Alisema mafunzo yaliyotolewa katika mkutano huo yamelenga kuwajengea watumishi uwezo katika maeneo mbalimbali ikiwemo maadili ya utumishi wa umma, mawasiliano kazini, afya ya akili, uwekezaji na ukuzaji wa vipaji mahali pa kazi.
Mkutano huo uliwakutanisha watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutoka mikoa 18 nchini ukiwa na kaulimbiu isemayo: “Mtumishi wa Umma Bora na wa Kisasa; Utaalamu, Ustawi na Mafanikio ya Kudumu.”














Post A Comment: