Na Mwandishi wetu- MBEYA

Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa Kitaifa wa Kuzuia, Kujiandaa, Kukabiliana na Kurejesha hali baada ya maafa ili kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira salama ya  kuepuka madhara makubwa yatokanayo na maafa.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Ofisi ya Mkoa wa Mbeya, Dkt. Noah Sikwese wakati akifunga mafunzo kwa Wajumbe Wateule wa Timu ya Kukabiliana na Dharura (RERT), Waatalamu wa Unendeshaji wa Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura (REOCC) katika Mkoa huo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa.

Dkt. Sikwese, amesema timu za kukabiliana na dharura zimejengewa msingi muhimu wa utendaji utakaowezesha Mkoa kuwa na uwezo wa kujiandaa na kukabiliana na matukio ya dharura kwa haraka  na ufanisi mkubwa .

“Timu hizi zitahusika katika kufanya tathmini za awali na za kina wakati wa maafa kubaini mahitaji halisi ya waathirika, pamoja na kuratibu upatikanaji wa rasilimali muhimu kwa ajili ya kukabiliana na athari za maafa,” alisema Dkt. Sikwese.


Pia, aliongeza kwamba mafunzo yamekuwa nyenzo muhimu katika kujenga na kuimarisha uwezo wa kitaalamu na kiutendaji kwa watumishi wanaohusika katika Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya dharura.

“Kuanzishwa kwa Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Mkoa wa Mbeya ni hatua muhimu katika kuimarisha uratibu wa shughuli za usimamizi wa maafa. Kituo hiki kitawezesha ufuatiliaji wa matukio  kwa ukaribu, ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa kwa wakati, pamoja na kuimarisha mawasiliano miongoni mwa wadau,” alieleza.

Sambamba na hilo Dkt. Sikwese alifafanua kuwa, utekelezaji wa mafunzo hayo ulianza katika Mikoa a Mwanza, Arusha, Dodoma, ambapo hatua za kuanzisha Vituo vya Operesheni na Mawasiliano ya Dharura pamoja na kuimarisha Timu za kukabiliana  na maafa zilianza kutekelezwa.


“Ni matarajio yangu mafunzo haya yataongeza ufanisi, uwajibikaji, ustahimilivu dhidi ya majanga katika Mkoa wetu wa Mbeya,”aliongeza.

Aidha, alitoa wito kwa wataalamu wote waliopatiwa mafunzo kuendelea kuyafanyia kazi maarifa na stadi, kudumisha nidhamu ya kazi na kujenga utamaduani wa ushirikiano wa kitaalamu huku akiwasisitiza kuendelea kufanya mazoezi ya mara kwa mara ya uokoaji na  utoaji wa huduma ya kwanza kwa majeruhi au waliofikwa na maafa.

“Usimamizi wa maafa ni jukumu letu sote, kila mmoja ashiriki sasa na kuchukua hatua katika eneo lake ili kuokoa na kulinda maisha, mali na mazingira,” alisisitiza Dkt. Sikwese.


Ikumbukwe kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa yam waka 2004 (Toleo la 2025) pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 202 imeipa jukumu la kuratibu masuala yote ya usimamizi wa maafa nchini.






MWISHO

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: