Wataalamu kutoka Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) wamehitimisha mafunzo maalum ya ulinzi na usalama dhidi ya mionzi kwa wafanyakazi wa Maweni Limestone Company. Mafunzo haya, yaliyofunguliwa na Meneja wa Idara ya Ubora wa kampuni hiyo, yalilenga kuwajengea uwezo wafanyakazi wanaoshughulika moja kwa moja na vifaa vya X-Ray Fluorescence (XRF) na nuclear gauges.

Kwa muda wa siku kadhaa, washiriki walipata nafasi ya kujifunza kwa kina kuhusu utambulisho wa mionzi ayonishi, kiasi cha mionzi na vipimo, matumizi ya mionzi, athari zake kiafya, kanuni za ulinzi, mfumo wa kisheria wa Tanzania, majukumu ya Afisa Usalama wa Mionzi (RSO), pamoja na usalama wa nyuklia na udhibiti wa usafirishaji haramu.

Katika hotuba ya kufunga mafunzo, wataalamu wa TAEC walisisitiza umuhimu wa kuimarisha utamaduni wa usalama kazini. “Tunataka kuona kila mfanyakazi akibeba jukumu la kulinda afya yake, wenzake na jamii kwa ujumla. Usalama wa mionzi si jambo la hiari, ni wajibu wa kitaifa,” alieleza Ndugu Mungubariki Nyaki, mkufunzi na msimamizi wa Ofisi ya TAEC Jijini Tanga.

Washiriki walionekana wenye shauku na ari ya kupeleka maarifa mapya kazini. Baadhi walikiri kuwa mafunzo haya yamewapa ujasiri wa kushughulika na vifaa vya mionzi kwa umakini zaidi, huku wengine wakisisitiza umuhimu wa kushirikiana na TAEC ili kuhakikisha viwango vya kitaifa na kimataifa vinazingatiwa.

Mafunzo haya pia yaligusia hatua za dharura endapo ajali za mionzi zitatokea, jambo lililowapa washiriki uelewa wa namna ya kukabiliana na changamoto kwa utulivu na ufanisi.

Kwa ujumla, kufungwa kwa mafunzo haya kumeacha taswira ya matumaini na uwajibikaji. Kampuni ya Maweni Limestone imeonyesha dhamira ya dhati ya kulinda wafanyakazi wake na jamii kwa kuhakikisha teknolojia za kisasa zinatumika kwa usalama na kwa manufaa ya Taifa.





Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OKULY BLOG

Post A Comment: