Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema Serikali inaendelea kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na upatikanaji wa umeme nchini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka 2026/2027.
Amesema hayo Aprili 23, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja za wabunge mara baada ya kuwasilishwa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati ya Mwaka 2026/2027.
Akijibu hoja hizo amesema Rais wa Jamuhurinya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kinara wa ajenda ya nishati safi ya kupikia, akilenga kufikisha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 huku akifafanua kuwa matumizi hayo yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi zaidi ya asilimia 28 kwa sasa, huku jitihada hizo zikilenga kulinda mazingira na afya za wananchi.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali imesambaza zaidi ya kilomita 56.4 za mabomba ya gesi asilia, mitungi ya gesi zaidi ya laki tatu, majiko ya gesi zaidi ya elfu 49 na majiko ya umeme zaidi ya elfu saba ambapo zaidi ya taasisi 55 zimepatiwa majiko ya nishati safi, huku mpango ukiwa kufikia taasisi zaidi ya 400.
Katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme vijijini zaidi ya visiwa 120 kati ya 143 tayari vimepata umeme wa sola kwa ruzuku ya asilimia 45 hadi 75 hatua inayolenga kuwaondoa wananchi katika matumizi ya vibatari na kuboresha maisha yao kwa ujumla.







Post A Comment: