Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amewataka watumishi wa Sekta ya Maji nchini kuongeza bidii, weledi na uwajibikaji ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Amesisitiza kuwa upatikanaji wa maji safi na salama ni nguzo muhimu ya maendeleo ya jamii na uchumi kukua hivyo kila mtumishi anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kujituma.

Akizungumza na Menejimenti ya Wizara ya Maji na RUWASA katika ukumbi wa Wizara ya Maji Mtumba, jijini Dodoma, Mhe. Aweso amebainisha kuwa mafanikio yanategemea mshikamano na ushirikiano wa dhati miongoni mwa watumishi. Amesisitiza  kuwa viongozi wanapaswa kuwa mfano bora kwa kuzingatia maadili ya kazi, uwazi na uwajibikaji, sambamba na kuimarisha mawasiliano katika  taasisi.

 Waziri Aweso amepongeza  menejimenti kwa kazi nzuri na ushirikiano katika suala la   ukaguzi wa kazi za Sekta ya Maji na kueleza , ni  mafanikio hayo yanaonyesha matumizi sahihi ya rasilimali za umma pamoja na usimamizi imara wa miradi ya maendeleo. Amewataka watumishi kuendeleza viwango hivyo na kujipambanua zaidi katika utendaji wao.

Amehimiza matumizi ya ubunifu pamoja na utekelezaji wa mkakati madhubuti wa kukabiliana na changamoto zilizopo, kukamilisha miradi kwa wakati na kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote. Amesema  kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuongeza ufanisi katika sekta.

Katika hatua nyingine, ameipongeza  RUWASA kwa juhudi kubwa za kushughulikia changamoto za wananchi kwa wakati, hatua inayochangia kuimarisha imani ya wananchi na kuboresha huduma ya maji  vijijini.

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji,  Mhandisi Mwajuma Waziri, amewataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana kwa karibu na kuweka mbele maslahi ya wananchi ili kuhakikisha huduma ya maji inaboreshwa na kuwa endelevu kwa manufaa ya sasa   na kizazi  kijacho.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: